1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yazindua baraza jipya la mawaziri

5 Novemba 2012

Somalia imetangaza baraza jipya la mawaziri na kuweka uwiano kati ya koo zinazohasimiana na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo mwanamke amechaguliwa kuwa waziri wa mambo ya nje.

https://p.dw.com/p/16csO
Serikali mpya ya Somalia
Serikali mpya ya SomaliaPicha: Reuters

Kuundwa kwa serikali hiyo mpya ni hitimisho la juhudi zilizosimamiwa na kanda na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa kurudisha udhibiti wa nchi kwa serikali kuu na kukomesha takriban miongo miwili ya mapigano ambayo yameuwa maelfu ya watu.Hapo mwezi wa Septemba Somalia ilimuapisha Rais Hassan Sheikh Mohamud aliechaguliwa katika uchaguzi wa kwanza wa aina yake tokea wababe wa kivita kumpinduwa dikteta wa kijeshi Mohamed Siad Barre hapo mwaka 1991 na kuliacha taifa hilo bila ya kuwa na serikali inayofanya kazi.

Miongoni mwa majukumu yanayomkabili Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon Saaid aliechaguliwa na Rais Mohamud kwa sababu ya kutoguswa na uhasimu ulioko baina koo za Somalia ni pamoja na kupambana na rushwa, uasi wa itikadi kali za Kiislamu na uharamia ulioko kwenye mwambao wa bahari ya Hindi ambayo ni njia muhimu ya meli.Saaid amewaambia waandishi wa habari kwamba kwa kuzingatia hali ilivyo hivi sasa amelichaguwa baraza dogo la mawaziri litakalokuwa na ufanisi ambalo litaiongoza serikali katika kipindi hiki kigumu na kufanikisha kupatikana kwa amani ya kuaminika.

Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon Saaid (mwenye miwani)akizungumza na Rais Hassan Sheikh Mohamud.
Waziri Mkuu Abdi Farah Shirdon Saaid (mwenye miwani)akizungumza na Rais Hassan Sheikh Mohamud.Picha: Reuters

Amemteuwa Fozia Yusuf Haji Aden kuwa waziri wa mambo ya nje na kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo mkubwa.Fozia anatokea jimbo lililojitangazia uhuru la Somaliland na aliwahi kuishi Uingereza kwa miaka mingi.Amesema uteuzi wake huo ni historia kwa nchi yake na ni ushindi hususan kwa wanawake wa Somalia.Mwanamke mwengine alieachaguliwa kwenye baraza hilo jipya la mawaziri ni Maryam Qasim Ahmed anayekuwa waziri wa maendeleo na masuala ya jamii.Awali alikuwa waziri wa wanawake.Saaid amewabakisha mawaziri watatu ambao walitumika katika serikali ya mpito ya zamani ya Rais Sheikh Sharif Ahmed miongoni mwao ni waziri wa ulinzi Abdihakim Haji Mohamud Fiqi.

Mwanamke wa Somalia akiwa na bendera ya nchi hiyo.
Mwanamke wa Somalia akiwa na bendera ya nchi hiyo.Picha: PHIL MOORE/AFP/Getty Images

Juu ya kwamba sio koo zote ndogo ndogo zimeweza kujumuishwa katika baraza hilo la mawaziri jambo ambalo ni muhimu kwa maisha ya kisiasa nchini Somalia, Saaid amesema wanajaribu kushughulikia matakwa, mashaka na matarajio ya wahusika mbali mbali nchini humo.Baraza hilo jipya la mawaziri itabidi liidhinishwe na bunge la Somalia.

Hatua ya vikosi vya Somalia, Ethiopia na vile vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika ya kuwatimuwa waasi wa Al Shabaab wanaoungwa mkono na kundi la Al Qaeda kutoka maeneo ya ngome zao kuu walizokuwa wamezidhibiti katika uasi wao wa miaka mitano, imewashajiisha Wasomali kurudi nchini kuijenga upya nchi yao.Lakini wanamgambo hao bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi mjini Mogadishu.

Wanajeshi wa Somalia wakiwa mjini Mogadishu.
Wanajeshi wa Somalia wakiwa mjini Mogadishu.Picha: REUTERS

Mwandishi. Mohamed Dahman/RTRU/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu