Somalia yautaka Umoja wa Mataifa kutuma majeshi nchi humo
2 Juni 2008Rais wa Somalia Abdullahi Yusuf amelitaka baraza la usalama la Umoja wa mataifa kupeleka wanajeshi wa kuweka amani wa Umoja wa mataifa katika nchi yake kabla ya kuondoka kwa wanajeshi wa Ethiopia wanaojaribu kuweka amani nchini humo.Ujumbe mzito wa baraza hilo la usalama la Umoja wa mataifa umejiunga na viongozi wa makundi yanayopingana ya Somalia katika kikao maalum cha kujaribu kutafuta maridhiano juu ya mzozo wa Somalia huko nchini Djibouti.Haya yote yanafanyika huku hali ya mambo nchini Somalia bado ikiwa ni tete.Jumapili rais wa Somalia aliponea chupuchupu jaribio la kutaka kumuua.
Rais Abdillahi Yusuf wa Somalia amesema kutaachwa pengo kubwa lakiusalama wakati wanajeshi wa Ethiopia watakapoondoka nchini Somalia hivyo basi ipo haja kwa baraza la usalama la Umoja wa mataifa kufikiria kupeleka wanajeshi wake katika nchi hiyo inayokabiliwa na hali tete.
Ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa ukiongozwa na balozi wa Afrika kusini katika Umoja wa mataifa Dumisani Kumalo pamoja na mwenzake wa Uingereza katika umoja huo John Sawers wamehudhuria kikao cha viongozi wa makundi yanayopingana ya Somalia nchini Djibouti kikao ambacho kinategemewa kutafuta njia za kumaliza mgogoro wa miaka kadhaa ambao umeisambaratisha nchi hiyo ya upembe wa Afrika.
Mazungumzo hayo ya Djibouti yanafanyika huku kukiwa na mapigano ya kila uchao kati ya vikosi vya wanajeshi wa Ethiopia na wapiganaji wa mahakama za kiislamu ambayo yamekuwa yakiendelea tangu mwaka mmoja uliopita na kusababisha mauaji ya raia elfu 6000 kwa mujibu wa makundi ya kutetea haki za binadamu na mashirika ya misaada.
Ni jana tu ambapo rais Abdillahi Yusuf Ahmed aliponea chuchupu kuuwawa baada ya shambulio la kombora lililoripuliwa karibu na ndege aliyokuwemo muda mchache kabla ya kuondoka kuelekea Djibouti.
Balozi wa Afrika Kusini katika Umoja wa mataifa anayeongoza ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa amesema shambulio hilo la jana ni dalili inayothibitsha umuhimu wa kuchukuliwa hatua za haraka juu ya suala la Somalia.
Ameongeza kusema ziara hiyo ya Ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa ni nafasi ya wasomalia kushirikiana na baraza la usalama la umoja wa mataifa na kuweka wazi juu ya hatua zinazopasa kuchukuliwa pamoja na kuendesha maridhiano.
Hata hivyo mambo sio rahisi katika majaribio ya kuutatua mzozo wa Somalia kwani baadhi ya viongozi wa makundi yenye itikadi kali wanasisitiza kuwa mazungumzo hayo ya upatanishi ni ya upendeleo na wanataka kwanza Ethiopia ijiondoe Somalia kabla ya kuanza mazungumzo ya dhati.
Lakini naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Alejandro Wolf anaipinga hatua hiyo ikiwa hakuna hatua mbadala itakayochukuliwa kudhibiti hali ya mambo katika taiafa hilo.
Wanajeshi wa Ethiopia waliingia Somalia mwaka 2006 kwa lengo la kuisaidia serikali ya mpito ambayo ni dhaifu na kuwatimua wapiganaji wa muungano wa mahakama za kiislamu ambao walikuwa wakidhibiti maeneo mengi ya kusini na kati mwa Somalia.Na tangu wakati huo wapiganaji hao wa mahakama za kiislamu wamekuwa wakiendesha mapigano ya kila siku dhidi ya wanajeshi wa kuweka amani wa Umoja wa Afrika katika mji mkuu wa Somalia Mugadishu.
Hatua kadhaa za majaribio ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Somalia zimeshindwa kufanikiwa tangu nchi hiyo ilipotumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1991 baada ya kuangushwa utawala wa rais Mohammed Siad Barre. Ingawa mara hii mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Somalia Ahmedou Ould Abdalla anasema kuna matumaini ya kupatikana maridhiano ikiwa ni baada ya miaka 17 ya vita.
Ujumbe huo wa baraza la Umoja wa mataifa utatembelea pia maeneo mengine tete barani Afrika ikiwa ni pamoja na Darfur,ChadJamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,na Ivory Coast.
►◄