Somalia yaondolewa marufuku ya kununua silaha
2 Desemba 2023Hilo linafanyika huku kukidumishwa marufuku ya mauzo kwa wapiganaji wa Kiislamu wa nchi hiyo.Jana jioni, Rais Hassan Sheikh Mohamud alinukuliwa akisema kuanzia sasa na kuendelea, nchi yao iko huru kununua aina yoyote ya silaha wanayotaka kutoka katika taifa lolote. Ameongeza kwa kusema silaha zikiwa katika udhibiti wa serikali, haziwezi kuwa kitisho kwa raia wa Somalia wala mataifa mengine.Umoja wa Mataifa mwaka 1992 uliweka zuio la kupokea silaha za aina zote nchini Somalia, ingawa katika miaka ya hivi karibuni Baraza la Usalama limepunguza vikwazo vya mauzo kwa serikali kuu.Serikali ya Somalia baada ya kupata mafanikio ya awali, katika mashambulizi yake ya Agosti 2022 dhidi ya Al-Shabaab, kunaonekana kuwa na mkwamo, hali inayosababisha mashaka juu ya uwezo wa serikali wa kukomesha uasi uliodumu kwa miaka 16 sasa wa kundi lenye uhusiano na al-Qaeda- Al Shabaab.