Somalia yanyemelewa tena na njaa
5 Julai 2012Hayo yameelezwa na shirika la misaada la Save the Children katika ripoti yake iliyotolewa siku ya Alhamis.
Ripoti hiyo imesema msaada mkubwa uliyotolewa mwaka jana, ulisaidia kuwaokoa watoto hao kutokana na njaa, lakini inaongeza kuwa mgogoro huo uliwalaazimu maelfu ya raia kuyahama makaazi yao, na hivyo kuharibu maisha yao na kuwaacha katika hatari ya kukumbwa na njaa huko mbele.
Imeongeza kuwa hivi sasa, mchanganyiko wa ukosefu wa makaazi, nvua zisizotosha na mavuno yanayotizamiwa kuchelewa, vinatishia kurudisha nyuma juhudi za ujenzi mpya kufuatia maafa hayo, kwa kuzingatia ukweli kwamba uwezo wa wasomali kukabiliana na uhaba wa chakula, ulipunguzwa kwa kiasi kikubwa na janga la mwaka jana.
Tahadhari za mapema
Tahadhari za mapema zinaonyesha kuwa upungufu wa nvua utasababisha kuchelewa kwa mavuno kusini kati mwa Somalia, eneo ambalo liliathiriwa zaidi na ukame wa mwaka jana.
Maelfu ya raia wa somalia wanaaminika kufariki mwaka huo, kutokana na kukithiri kwa njaa iliyosababishwa na ukame, na vita. Ingawa janga la njaa lilitangazwa kuisha mwezi Februari mwaka huu, hali mbaya ya ukame bado inaendelea katika maeneo mengi ya nchi hiyo.
Sonia Zambakides kutoka Programu ya Somalia ya Save the Children, alisema watu milioni 1.4 walioyahama makaazi yao kutokana na njaa na vita, wako hatarini kuathirika kwa sababu tegemeo lao ni mavuno mazuri ambayo yanasaidia kupunguza gharama za vyakula. Save the Children imeomba msaada wa dharura ili kusaidia waathirika.
Umoja wa Mataifa nao waonya
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa baadhi ya maeneo ya kusini mwa Somalia, ambako ndiko kuna mapambano baina ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika dhidi ya kundi la al-Shabaab, yako hatarini kuserereka kufikia kiwango cha dharura.
Mtandao unaotoa tahadhari ya mapema ya njaa, unaosaidia na serikali ya Marekani, Femine Early Warning Systems Network, umeonya kuwa, nvua muhimu kwa mavuno zimechelewa na mgawanyo wake haukuwa mzuri, lakini likaongeza kuwa halitarajii kurudi katika hali ya njaa.
Zambakides amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kushughulikia sababu za muda mrefu zinazopelekea kuwepo njaa nchini Somali, vinginevyo ijiandae kuona hali mbaya zaidi huko mbele. Amesema suluhu sio kuitikia dharura, bali ni kuweka mazingira ya kuondoa tatizo hili katika muda mrefu.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman