Somalia yajipatia waziri mkuu mpya
25 Novemba 2007Baidoa:
Bunge la Somalia lililokutana jana mjini Baidoa,kusini mwa nchi hiyo,limemuidhinisha kwa sauti moja waziri mkuu mpya Nour Hassan Hussein,saa 48 tuu baada ya kuteuliwa na rais Abdullah Yusuf.Mtangulizi wake,Ali Mohammed Gedi alijiuzulu mwishoni mwa mwezi uliopita kufuatia mvutano wa kisiasa pamoja na kiongozi wa taifa.Rais Abdullah Yussuf amemsihi waziri mkuu mpya aunde haraka serikali yake.”Nnaamini serikali mpya itatekeleza majukumu yake katika kipindi cha miaka miwili ijayo” amesema rais Abdullah Yusuf.Waziri mkuu Nour Hassan Hussein,maarufu kwa jina la Nur Adde,ni kanali wa zamani aliyetumikia vikosi vya polisi wakati wa enzi za Mohammed Siad Barre.Husseion aliyesomea sheria nchini Italy ni makamo mwenyekiti wa shirika la Hilal Nyekundu la Somalia.