1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia, mwito wa vikwazo na kurejea nyumbani majeshi ya Ethiopia

Nijimbere, Gregoire4 Juni 2008

Makundi ya kiraia kutoka Somalia yametoa mwito mjini Djibuti kwa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa liyachukulie vikwazo makundi yanayokaidi mazungumzo na majeshi ya Ethiopia yarudi nyumbani.

https://p.dw.com/p/EDR6
Maharamia waliokamatwa SomaliaPicha: picture-alliance/dpa

Katika taarifa ya pamoja, makundi hayo ya kiraia kutoka Somalia, yameliomba Baraza la usalama la usalama la Umoja wa mataifa kuyachukulia hatua kali makundi ya waasi yanapinga kushiriki kwenye mazungumzo ya kusaka amani. Makundi hayo ni pamoja na Islamist al Shabaab na muungano wa makundi ya kiislamu yanayosaidiwa na Eritrea na ambayo yalifukuzwa mjini Mogadishu na majeshi kutoka Ethiopia mwaka mmoja na nusu uliopita. Makundi hayo ya waasi yalipinga kushiriki kwenye mazungumzo ya ana kwa ana na serikali kabla ya majeshi kutoka Ethiopia kuondoka Somalia.

Dai hilo la kuondolewa kwa vikosi kutoka Ethiopia kutoka Somalia limeungwa mkono na makundi hayo ya kiraia katika taarifa yao. Makundi hayo yanawajumuisha wawakilishi wa koo za kisomali, watetezi wa haki za binaadamu, wanaharakati wa amani, wafanyabiashara na wawakilishi wa wanawake na raia wa Somalia wanaoishi katika nchi za nje.

Kwa upande wake mpatanishi wa zamani katika mzozo wa Somalia kwa ajili ya mamlaka ya ushirikiano wa maendeleo IGAD Bethuel Kiplagat, amesema kitu cha dharura ni kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na halafu kuwatuma wanajeshi wa Umoja wa mataifa wa kulinda amani nchini Somalia. Laa sivyo amesema hakuna mazungumzo ya amani yatakayofanikiwa bila utulivu mjini Mogadishu.

Kiplagat amezidi kuelezea kuwa yale makundi ya kiislamu yanayopinga kushiriki katika mchakato wa amani yatapoteza imani ya raia na kukituma kikosi cha kijeshi cha Umoja wa mataifa nchini Somalia kutatoa fursa kwa majeshi ya Ethiopia kuondoka kutoka Somalia.

Kwa maoni ya mpatanishi huyo wa zamani kuhusu mzozo wa Somalia, pamoja na kudhaminia usalama, kikosi hicho cha Umoja wa mataifa nchini Somalia kinahitajika kusaidia katika shughuli za misaada ya dharura kwa wahanga wa vita.

Kwa hakika zaidi ya raia wa Somalia milioni 2 wanahitaji misaada ya dharura na Umoja wa mataifa umeonya kwamba idadi hiyo inaweza kupanda na kufikia milioni 3 na nusu kutokana na mfumko mkubwa wa bei nchini Somalia, zikiwemo bei za chakula.


Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa waliosimamia mazungumzo hayo, waliyasikiliza makundi yote yalioshiriki bila hata hivyo kutangaza msimamo wao na kuondoka kuelekea Sudan. Isipokuwa tu juu ya swala la uharamia kwenye pwani ya Somalia, iliamuliwa kila nchi yaruhusiwa kutumia uwezo wake kupambana na uharamia katika eneo hilo.