Somalia: Msaada wa chakula washirika la Msalaba Mwekundu wazuiliwa
16 Desemba 2011Wakaazi wa mji wa Baidoa, eneo ambalo ni ngome ya kikundi cha Al-Shabaab wamesema wameona wapiganaji wa kiisilamu wakishusha shehena ya vyakula hivyo katika magari na kuvipeleka katika maghala yao.
Habari kutoka kwa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada zinasema pia kwamba Al-Shabaab walitaka kukaguwa ubora wa chakula hicho, lakini wakilenga msafara wa magari ya shirika la msalaba mwekundu.
Labda hatua hiyo ya Al-shaabab ni kutokana na kikundi hicho cha waislamu kupiga marufuku mashirika ya misaada kufanya kazi nchini Somalia, hasa maeneo yanayoshikiliwa na Al- Shabaab.
“wanajifanya kutaka kukaguwa chakula, lakini agenda yao ni nyengine,” alisema mfanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Shirika la kimataifa la msalaba mwekundu liliripoti mwezi Agosti mwaka huu kuwa lina mpango wa kuongeza ugawaji wa vyakula nchini Somalia, hasa katika eneo ya kusini mwa Somalia kuwasaidia watu zaidi ya milioni 1 na laki moja ambao wameathirika na ukame na vita vya muda mrefu.
Kwa muda sasa, mara nyingi shirika na msalaba mwekundu limekuwa likifanya kazi zake vizuri katika maeneo ya kusini na kaskazini mwa Somalia, ambako yanashikiliwa na makundi ya kiislamu yenye uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al-Shabaab, na si kawaida kwa magari ya shirika hilo kusimamishwa.
Msafara wa magari bado unashikiliwa katika eneo ya Shebelle baada ya kusimamishwa mwezi huu.
“Wapiganaji wa Al-shabaab wametuzingira, hawatoachilia magari yetu mpaka uamuzi utoke kwa viongozi wao,” dereva mmoja wa shirika hilo la misaada alisema kwa simu bila kutaja jina lake.
Msafara huo wa magari ulikuwa ukisafirisha shehena ya mchele, mafuta ya kupikia, na maharage kwenda katikati ya Somalia kabla ya kusimamishwa na kuzuiliwa.
Magari mengine yalisimamishwa eneo la Gedo, kusini kwa Somalia, kama ambavyo taarifa kutoka na mashirika ya misaada kutoka Nairobi, zinasema.
Bado wananchi wengi nchini Somalia wanakabiliwa na shida ya ukosefu wa chakula kutokana na kukosekana na vua kwa muda mrefu pamoja na vita, huku makundi ya kiislam hasa la al shabaab likiwa hakina msimamo juu ya mashirika ya kutoa misaada.
Mwandishi: Salma Said
Mhariri: Othman Miraji