1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia kumchagua rais mpya

Eric Kalume Ponda30 Januari 2009

Bunge la Somalia linapiga kura leo kumchagua rais mpya atakayechukua mahala kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdullahi Yusuf Ahmed aliyejiuzuli mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/Gjs6
Raia wa Somalia wakisubiri kwa hamu matokeo ya uchaguzi wa Urais hivi leo.Picha: AP


Wabunge hao wanaokutana mjini Djibouti, Eritrea kwa kuhofia usalama ndani ya nchi yao, wanabeba dhamana kubwa ya kuimarisha hali ya usalama katika taifa hilo ambalo halijakuwa na serikali dhabiti tangu kuanguka kwa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa kiimla Mohammed Siad Barre miaka 18 iliyopita.


Uchaguzi huo umefanyika wiki moja tu baada ya bunge hilo kupanuliwa ili kuwajumuisha wabunge kutoka muungano wa vyama vya upinzani vinavyozingatia siasa za mrengo wa kadri Islamic Alliance for Re-Liberation of Somalia(ARS).

Bunge hilo sasa lina linajumla ya idadi ya wabunge 550 baada ya kuapishwa wiki iliyopita kwa wabunge hao wa chama cha ARS mjini Djibouti,katika juhudi za kuyaleta karibu makundi ya upinzani kupitia mpango wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Kuna jumla ya wagombea 14 wa kiti hicho cha Urais, ingawa kinyanganyiro kinatarajiwa kuwa baina ya waziri mkuu Nur Hassan Hussein na kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani (ARS) Sheikh Sharif Sheikh.


Sheikh Sharif pia ndie kiongozi wa chama cha Mahakama za Kiislamu ICU, ambacho kilichukua usimamizi wa taifa hilo mwaka wa 2006 kabla ya kutimuliwa na wanajeshi wa Ethiopia.


Viongozi hawa wawili wameonyesha haiba kubwa miongoni mwa wafuasi wao kutokana na msimamo wao wa kutaka usalama udumishwe nchini humo, ingawa wanatofautiana kuhusu mfumo wa serikali na utawala.


Sheikh Sahrif anataka kudumisha na kuimarisha utawala unaozingatia shaqria za Kiislamu,huku waziri mkuu akiimarisha jeshi la nchi hiyo na kuvinja mfumo wa utawala wa kimbari anaotaja kuwa chanzo cha machafuko nchini Somalia.


Sheikh Sahrif pia anasifiwa na jamii ya kimataifa kwa juhudi zake za kibinadamu ingawa hajakuwa na ufusai mkubwa kutoka kwa kabila lake. Hata hivyo wabunge waliokuwa wakimuunga mkono rais wa zamani Abdallahi Yusuf wanasema kuwa watamuunga mkono Sheikh Sharrif wakati wa uchaguzi huo.


Itakumbukwa kwamba waziri mkuu Nur Hassan Husein walitofautiana vikali na rais huyo wa zamani Abdullahi Yusuf, tofauti ziliyopelekea kujiuzulu kwake na kuitikisa zaidi serikali hiyo changa.


Kwa wakati huu serikali inadhibiti eneo ndogo la mji mkuu wa Mogadishu kufuatia mapigano makali baina ya wapiganaji wa makundi ya Kiislamu na serikali.Watu 30 waliuawa kufuatia mashambulio makali yaliyotokea jana baina ya makundi hayo ya Kiislamu.


Hata mgawanyiko ndani ya makundi hayo ya wapiganaji wa kiislamu bado unatajwa kuwa changamoto kubwa kupatikana kwa amani ya kudumu katika taifa hilo.


Wengi wanaamini bila ya kuhusishwa kwa kiongozi wa mrengo wenye siasa kali katika kundi hilo la Mahakama za Kiislamu Sheikh Hasaan Dahir anayeishi uhamishoni nchini Eritrea, huenda juhudi za kupatikana kwa amani ya kudumu nchini Somalia ikasalia ndoto tu.


Hali ya usalama nchini Somalia imeendelea kuzorota baada ya wanajeshi wa Ethiopia kuondoka bila ya kuzungumzia mafanikio yoyote.


Ukosefu wa usalama nchini Somalia umesababisha kuongezeka kwa visa vya uharamia katika pwani ya nchi hiyo na kutishia safari za vyombo vya habarini.Zaidi ya Meli kadhaa bado zinazuiliwa na maharamia baada ya kutekwa nyara katika pwani ya nchi hiyo.


Ponda/Afp-Reuters