1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia huenda ikahalalisha ndoa za utotoni

12 Agosti 2020

Hasira inazidi kuongezeka nchini Somalia wakati bunge likipanga kuujadili muswada wa sheria ambayo itaruhusu ndoa za watoto mara baada ya kubalehe, na kuruhusu ndoa za lazima ilimradi familia itoe ridhaa yake. 

https://p.dw.com/p/3gptq
Äthiopien Kinderehe child marriage
Picha: picture alliance/Godong

Muswada huo unatajwa kuwa mabadiliko makubwa katika jitihada za mashirika ya kiraia za kuwasilisha pendekezo la sheria ya kuwalinda zaidi wanawake katika moja ya mataifa ya kihafidhina zaidi duniani.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu vurugu za kingono katika maeneo ya migogoro, Pramila Patten, amesema muswada huo mpya wa makosa yanayohusiana na ngono, "utakuwa ni pigo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kingono nchini Somalia na duniani kote" na unapaswa kuondolewa haraka".

Kulingana na tathmini ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014-2015, zaidi ya asilimia 45 ya wasichana nchini Somalia tayari wameolewa katika umri mdogo wa chini ya miaka 18.

Somalia ilikubaliana na Umoja wa Mataifa mwaka 2013 kuboresha sheria zake zinazohusiana na vurugu za kingono, na baada ya miaka mitano ya juhudi, muswada wa makosa ya kingono uliidhinishwa na baraza la mawaziri na kutumwa bungeni.

Bangladesch Kinderheirat
India ni miongoni mwa mataifa yanayoendeleza ndoa za mapemaPicha: Getty Images/A. Joyce

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa amesema lakini mwaka uliopita, spika wa baraza la watu aliurejesha, katika mchakato ambao huenda uliubadilisha kutoka sheria iliyokuwepo, akitaka "marekebisho makubwa".

Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Michele Bachelet alisema wiki hii kwamba, muswada huo mpya "unahatarisha kuhalalisha ndoa za utotoni, miongoni mwa vitendo vingine vyenye kutia mashaka na lazima uzuiliwe kupitishwa". Mkuu huyo ameonya kwamba endapo utapitishwa, itakuwa ni ishara mbaya kwa mataifa mengine katika ukanda huo.

Maelfu ya raia nchini humo wameanza kusambaza malalamiko dhidi ya muswada huo kupitia mitandao ya kijamii, wakati taifa hilo likiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana siku ya Jumatano. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia katika taarifa yake, umeuelezea muswada huo usio na msingi na kulitaka bunge kuwasilisha tena muswada wa awali, ukiongeza kuwa "utakuwa ni muhimu katika kuzuia na kuhalalisha makosa yote ya kingono".

Balozi wa Ungereza nchini Somalia, Ben Fender ameandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba, ni muda muafaka kwa wabunge wa taifa hilo kuamua juu ya mustakabali wa Somalia".

Muswada huo tata unakuja wakati makundi ya harakati za wanawake yakishikwa na wasiwasi kwamba janga la virusi vya corona na zuio la kusafiri nchini Somalia, vimezidisha ukatili na ukeketaji dhidi ya wanawake.