1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia hali ya usalama inazorota Mogadishu

2 Agosti 2007

Takriban watu 10 wameuwawa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu kufuatia mashambulio ya watu wanaoshukiwa kuwa ni wapiganaji mahakama za kiislamu.

https://p.dw.com/p/CHA6
Mapigano ya Mogadishu
Mapigano ya MogadishuPicha: picture-alliance/ dpa

Watu hao walifyetua roketi na makombora dhidi ya vikosi vya usalama vya Somalia.

Katika muda wa wiki nzima mji mkuu wa Somalia Mogadishu umeshuhudia ongezeko la mashambulio ya wapiganaji ambao wamekuwa wakilenga vikosi vya wanajeshi wa serikali na washirika wao Ethiopia pamoja na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika kutoka Uganda.

Kiasi cha watu 10 wameuwawa kwenye uvamizi uliotokea usiku dhidi ya kituo cha polisi kaskazini mwa mji wa Mogadishu katika mji wa Daynile.

Mtu mmoja aliuwawa wakati mshambuliaji alipovurumisha kombora katika mkahawa mmoja maarufu kwa maafisa wa kijeshi kusini mwa mji huo.

Polisi wanasema mashambulio hayo yamefanywa na watu wasiojulikana.Afisa mmoja wa polisi mjini Mogadishu Abdullahi Haasan amesema ni wajibu wa wakaazi kuzuia wahalifu kujificha miongoni mwao.

Wanajeshi tisa wa Somali walijeruhiwa kufuatia shambulio la gruneti nje ya mkahawa wa Madina.

Mbunge Hussein Bantu anayehudhuria vikao vya bunge mjini Baidoa anasema serikali ya mpito inaelewa fika malengo ya wapiganaji wakiislamu lakini hivi karibuni mashambulio yao yatafika mwisho

Mji mkuu Mogadishu umekuwa ukikabiliwa na ghasia tangu mwezi Januari wakati serikali ya mpito na wanajeshi wa Ethiopia walipowatimua wapiganaji wakiislamu ambao walidhibiti maeneo mengi ya kusini mwa Somalia kwa muda wa miezi sita mwaka jana.

Wapiganaji hao sasa wanalaumiwa kwa kuanzisha mbinu mpya za mapigano zinazofanana na zile zinazofanyika Iraq kutega mabomu kando ya barabara,kujitoa muhanga na mauaji ya kinyama.Vitendo hivi vimesababisha wakaazi wengi wa mji huo kukimbia na kushindwa kurudi tena kwani kila uchao hali haibadiliki.

Mbunge Hussein Bantu anasema wakimbizi wengi wameweza kurudi nyumbani isipokuwa wachache ambao wanaoishi kwenye kitovu cha Somalia Mogadishu ndio walioshindwa kufanya hivyo.

Wakati ghasia zinaendelea katika mji huo mazungumzo ya kutafuta suluhu yanaonekana kutosonga mbele kwani hadi sasa kundi la mahakama za kiislamu limekataa kujiunga na mchakato huo.