1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Solana aitembelea Afghanistan.

Halima Nyanza21 Julai 2009

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, leo anaitembelea Afghanistan kwa mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, na baadhi ya wapinzani wa Rais huyo wanaohiriki katika uchaguzi wa nchi hiyo unaofanyika mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/IuTk
Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO Javier Solana.Picha: AP

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya, mkuu wa Sera za Nje wa umoja huo, Javier Solana, na viongozi wa kisiasa nchini Afghanistan watajadili maendeleo ya hivi karibuni yaliyopatikana nchini humo na katika kanda hiyo pamoja na kuzungumzia uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.


Solana atakutana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Afghanistan, Rangin Dadfar Spanta, na kiongozi wa waangalizi wa Chaguzi wa Umoja wa Ulaya nchini humo, na pia kusisitizia uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya katika juhudi za kuijenga upya na kuiimarisha Afghanistan.


Msemaji wa Umoja wa Ulaya amethibitisha kuwasili kwa Javier Solana leo kufuatia mazungumzo yaliyofanyika nchini Pakistan, ambapo wapiganaji wa kiislamu wamekimbilia baada ya uvamizi uliofanywa na majeshi yanayoongozwa na Marekani nchini Afghanistan kuung'oa madarakani utawala wa Taliban mwishoni mwa mwaka 2001.


Ziara hiyo ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, inakuja wakati ajali nyingi zikiwakumba wanajeshi wa nchi za magharibi nchini Afghanistan, huku Marekani na Washirika wake wa Ulaya wakiongeza vikosi kuweza kupambana na wapiganaji wa Taliban, kuunga mkono majeshi ya ulinzi ya Afghanistan pamoja na kuweka usalama kwa ajili ya uchaguzi wa nchi hiyo unaofanyika Agusti 20.


Umoja wa Ulaya umetuma timu yake ya waangalizi mwezi huu nchini Afghanistan kujiandaa na uchaguzi wa Rais na wa majimbo.


Waangalizi wengi wa uchaguzi wana wana wasiwasi juu ya kuendeshwa uzuri zoezi hilo la uchaguzi katika nchi hiyo ambayo bado, kwa kiasia kikubwa, inadhibitiwa na makundi ya wapiganaji.

Wakati mkuu wa sera za Nje wa Umoja wa Ulaya akitarajia kukutana na viongozi wa Afghanistan leo nchini humo, maafisa wa nchi hiyo wamesema kwamba Wapiganaji 13 wa Taliban pamoja na wanajeshi wa nchi hiyo wamekufa katika mashambulio yaliyotokea kwenye mjini miwili mashariki mwa Afghanistan.


Polisi nchini humo wamefahamisha kuwa washambuliaji wa kujitoa mhanga wapatao watano na wanajeshi watano wa Afghanistan wamekufa katika shambulio lililotokea leo.


Na katika shambulio la pili polisi wamesema washambuliaji wawili wa kujitoa mhanga waliokuwa ndani ya pikipiki na polisi mmoja wamekufa katika mji wa mashariki wa Jalalabad baada ya kushambuliana kwa risasi.


Kabla ya Kutembelea Afghanstan, Bwana Solana aliitembelea pia Pakistan na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo, akiwemo Waziri Mkuu, Yousuf Raza Gilani.


Mwandishi: Halima Nyanza (afp, ap)

Mhariri: Miraji Othman