Snowden afunguliwa mashitaka
22 Juni 2013Chanzo nchini Marekani ambacho hakikutajwa pia kimesema kuwa serikali ya Marekani inapanga kumrejesha nyumbani Snowden kutoka Hong Kong, ambako anaaminika kuwa amejificha. Gazeti la The Washington Post limesema pia kuwa kesi hiyo iliyowasilishwa mahakamani na waendesha mashitaka inamtuhumu Snowden kwa upelelezi, wizi na utoaji wa mali ya serikali. Mashitaka yote yana adhabu ya hadi miaka kumi gerezani.
Kesi hiyo ilifunguliwa mnamo Juni 14, siku tano baada ya jina la Snowden kujitokeza kama mfichuaji wa habari kuhusu mipango mwili ambayo Shirika la Ujasusi NSA lilikusanya data za simu n mtandao wa internet ili kugundua njama za mashambulizi ya kigaidi.
Snowden anaweza kupinga kuhamihwa kwake
Kesi hiyo huenda ikawa sehemu muhimu ya juhudi za serikali ya Marekani kufanikisha uhamisho wa Snowden kutoka Hong Kong, shughuli ambayo huenda ikageuka na kuwa vita vya muda mrefu vya kisheria. Snowden anaweza kupinga uhamisho wake kwa misingi ya kunyanyaswa kisiasa. Kwa ujumla, muafaka wa uhamisho baina ya Marekani na Hong Kong hautakuwa na idhini ya kumhamisha mtu kwa makosa ya kisiasa. Haijakuwa wazi kama Marekani imetuma ombi rasmi kwa Hong Kong kumhamisha Swnoden, wakati nayo Hong Kong ikisalia kimya kuhusiana na suala hilo.
Sheria ya Upelelezi ni kosa la kisiasa. Serikali ya Obama sasa imetumia sheria hiyo katika kesi nane za uhalifu katika juhudi za kujaribu kutokomeza ufichuaji wa habari za siri. Katika mojawapo ya kesi hizo, Afisa wa Jeshi Bradley Manning alikiri kutuma zaidi ya ripoti za kijeshi laki saba, habari za siri za kidiplomasia na maelezo mengine kwa mtandao wa udukuzi wa Wikileaks. Kesi yake inaendelea katika mahakama ya kijeshi.
Marekani na Hong Kong zina muafaka
Seneta Bill Nelson, mwanachama wa Kamati ya Baraza la Seneti kuhusu huduma za Jeshi ameikaribisha hatua ya kumfungulia mashitaka Snowden. Amesema kosa alilofanya ni la uhaini na hivyo anataraji kuwa serikali ya Hong Kong itaweza kumtia mbaroni na kumkabidhi kwa Marekani.
Marekani na Hong Kong hushirikiana kuhusu masuala ya utekelezaji wa sheria na zina muafaka unaoziwezesha nchi hizo mbili kuwasalimisha wahalifu. Hata hivyo haki za Snowden za kukata rufaa zinaweza kuchelewesha shughuli yoyote ya kutaka kumkabidhi kwa Marekani.
Mafanikio au kushindikana kwa mchakato wa kumhamisha kutalingana na kile mshukiwa atashitakiwa nacho chini ya sheria ya Marekani, na jinsi inavyoambatana na sheria ya Hong Kong chini ya muafaka wa nchi hizo mbili.
Mwandishi. Bruce Amani/AP
Mhariri: Sekione Kitojo