1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SIPRI: Vichwa vya nyuklia duniani ni 16,300

Josephat Nyiro Charo16 Juni 2014

Ripoti ya taasisi ya kimataifa ya amani, SIPRI, iliyotolewa leo (16.06.2014) Stockholm inasema vichwa vya nyuklia vimepungua kufikia 16,300 mwaka huu kwa kuwa Marekani na Urusi zilipunguza utengenezaji wa silaha hizo.

https://p.dw.com/p/1CJ0C
Pakistan Atombombe Rakete in Islamabad
Picha: FAROOQ NAEEM/AFP/Getty Images

Vichwa vya nyuklia vimepungua kufikia 16,300 mwaka huu kwa sababu ya hatua ya Marekani na Urusi kupunguza utengenezaji wa silaha hizo kufuatia mkataba baina ya nchi hizo mbili wa kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia, START, uliosainiwa mwaka 2011. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya kimataifa ya amani, SIPRI, iliyotolewa leo mjini Stockholm Sweden.

Idadi ya vichwa vya nyuklia ilipungua kwa 970 ikilinganishwa na mwaka jana. Makadirio hayo yanajumuisha vichwa vya nyuklia vinavyoweza kutumiwa, vilivyo katika maghala ya silaha au vile ambavyo vinasubiri kuharibiriwa. Dola mbili kubwa zenye silaha za nyuklia - Marekani na Urusi - kwa pamoja zinamiliki zaidi ya asilimia 90 ya silaha zote za nyuklia duniani. Marekani inakadiriwa kumiliki vichwa 7,300 vya nyuklia huku Urusi ikiwa na 8,000.

Kile Shannon, mmoja wa watayarishaji wakuu wa ripoti hiyo mpya ya SIPRI amesema kwa kuzingatia silaza za nyuklia ambazo bado zipo, makubaliano ya kuzipunguza silaha hizo bado hayajatekelezwa kikamilifu na mapunguzo ni madogo.

"Silaha nyingi za nyuklia zinazopunguzwa au kuharibiwa sasa ni vichwa vya nyuklia vya tangu enzi ya vita baridi. Upunguzaji wa matumizi ya silaha za nyuklia umekuwa mdogo. Silaha 16,000 za nyuklia duniani bado ni idadi kubwa mno."

Ripoti ya taasisi ya SIPRI imesema jumla ya nchi tisa zinaaminiwa kumiliki silaha za nyuklia. Mbali na Marekani na Urusi, nyingine ni Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini. Imebainika kwamba Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa kwa jumla zina silaha 4,000 za nyuklia zinazoweza kutumika.

Hali ya kuvunja moyo

Anette Schaper, Mkuu wa miradi na mtaalamu wa udhibiti wa silaha za nyuklia katika wakfu wa amani na utafiti wa mizozo wa Hessen mjini Frankfurt, Ujerumani, amesema matokeo haya yanatokana na uhusiano mgumu kati ya Marekani na Urusi kama ilivyokuwa zamani. Aliyefikiria kwamba kuanza kutekelezwa mkataba wa kupunguza matumizi ya silaha za nyuklia kati ya Marekani na Urusi mwaka 2011, START, kungeufanya ulimwengu kuwa eneo huru kutokana na silaha za nyuklia alitarajia makuu.

NO FLASH Symbolbild USA geben Zahl ihrer Atomsprengköpfe bekannt
Vichwa vya nyuklia vya MarekaniPicha: picture alliance/abaca

"Hali jumla inavunja moyo. Kulikuwa na ulazima wa kuimarisha uhusiano na Urusi na kuipa nafasi zaidi na kuisikiliza inachosema katika baraza la jumuiya ya NATO na Urusi."

Mtaalamu huyo wa Ujerumani hajavunjwa moyo tu na ukweli kwamba kuna silaha za nyuklia Ujerumani, bali pia na hatua ya jumuiya ya kujihami ya NATO mpaka sasa kushindwa kuziondoa na kuziangamiza silaha hizo.

Dola zaendelea kuboresha silaha

Watafiti wa SIPRI wamesema dola zenye nyuklia zimeendelea kuimarisha na kuboresha silaha zao za nyuklia na mifumo ya ugavi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Marekani imetenga dola bilioni 350 kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza silaha zake za nyuklia katika miaka kumi ijayo, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika nyambizi mpya na kudurusu makombora mapya na ndege za kuvurumisha makombora ya masafa marefu.

Ripoti hiyo inasema Urusi, mbali na kuboresha makombora yake, inatengeneza pia aina mpya ya nyambizi inayoweza kuweza kuvurumisha silaha za nyuklia baharaini.

India na Pakistan zimeendelea kuboresha makombora yao na pia kutengeneza nyenzo za nyuklia kwa matumizi ya kijeshi. India imekadiriwa kumiliki vichwa kati ya 90 na 110 vya nyuklia, Pakistan kati ya 100 na 120, huku Israel ikibakia na shehena ya vichwa 80 kwa mujibu wa SIPRI. Shannon amesema mpango wa nyuklia wa Isreal unaonekana kuwa imara. Hata hivyo amesema Israel inasubiri kuona kitakachotokea nchini Iran. Kama Iran itatengeneza bomu la nyuklia, hatua hiyo inaweza kuwa na ushawishi kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia za Israel.

Iskander Rakete
Picha: picture-alliance/dpa

Idadi ya vichwa vya nyuklia vya China ni 250, 190 kati ya hivyo vikiwa ni kwa ajili ya makombora ya ardhini na ndege zake za kivita. Korea Kaskazini, ambayo ilifanya jaribio la nyuklia mnamo mwaka 2006, inaaminiwa kuwa na vichwa kati ya 6 na 8 kwa mujibu wa taasisi ya SIPRI.

Mwandishi: Jeppesen, Helle

Tafsiri: Josephat Charo

Mhariri: Daniel Gakuba