1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sintofahamu baada ya ushindi wa Maathir

10 Mei 2018

Mahathir Mohamad aliyeshinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu nchini Malaysia uliofanyika siku ya Jumatano, ataapishwa muda wowote hii leo kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo na kuunda serikali mpya licha ya sintofahamu.

https://p.dw.com/p/2xTNj
Mahathir Mohamad, ehemaliger Premierminister Malaysias
Picha: picture alliance/MAXPPP

Mahathir Mohamad ameshinda kwa kishindo uchaguzi mkuu nchini Malaysia, na kuweka historia ya kuwa waziri mkuu wenye umri mkubwa zaidi duniani, akiwa na umri wa miaka 92. Mahatir anatarajiwa kuapishwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo wakati wowote kuanzia sasa na kuufikisha mwisho utawala wa muungano wa Barisan Nasional ulioitawala Malaysia tangu ilipojipatia uhuru waka mnamno mwaka 1957. 

Muda mfupi baada ya Mahathir kutangaza kushinda kwenye uchaguzi huo, alisema mfalme wa Malaysia atasaini barua ya kumthibitisha kuwa waziri mkuu wa taifa hilo, katika sherehe zitakazofanyika kwenye kasri hilo lililoko katika mji mkuu, Kuala Lumpur hii leo. 

Lakini, mamlaka la kasri hilo la kifalme zimesema, huenda hakutakuwepo na shughuli kama hiyo na msemaji wa Mahathir, kiongozi mkongwe mwenye umri wa miaka 92, na waziri mkuu wa zamani amesema, hajasikia taarifa zozote kutoka kwenye kasri hilo na hakuwa na mpango wa kwenda huko.  

Hata hivyo Maathir,  kiongozi huyo wa zamani kiimla, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba wana haki dhahiri ya kuunda serikali mpya na kusisitiza kwamba anatakiwa kuapishwa leo kuwa waziri mkuu, kwa kuwa muungano wa upinzani unaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge. 

Malaysia Mahathir Mohamad
Muungano wa upinzani wa Mahathir unaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge.Picha: picture alliance/ZUMAPRESS

Upinzani una uungwaji mkono mkubwa.

Muungano wa upinzani ulioongozwa na Mahathir umeshinda wingi wa viti unaotakiwa katika kuunda serikali mpya kwenye uchaguzi uliofanyika siku ya Jumatano, na ni ushindi mkubwa unaohitimisha utawala wa muda mrefu wa muungano ambao aliwahi kuuongoza. 

Wamalaysia walishangilia ushindi huo wa Mahathir ambao haukutarajiwa dhidi ya waziri mkuu Najib Razak, ambaye umaarufu wake umeshuka kufuatia kuongezeka kwa gharama za maisha na kashfa kubwa ya ufisadi wa mabilioni ya fedha yaliyopelekwa nje ya nchi.  

Waziri huyo mkuu Najib Razak, aliyeongoza muungano unaoongoza serikali wa National Front ulioshindwa vibaya kwenye uchaguzi huu, amesema anakubaliana na matokeo. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliopeperushwa mubashara kupitia televisheni, amesema yeye na washirika wake wamekubaliana na matakwa ya raia.

Razak awataka raia kuwa na subira wakisubiri maamuzi ya mfalme.

Malaysia Wahl Premierminister Najib Razak
Waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak, amesema amekubaliana na matokeo ya kushindwa. Picha: Reuters/A. Perawongmetha

Mahathir aliwahi kuliongoza taifa hilo la Kusini mashariki mwa Asia kwa miaka 22 na kurejea kwake kwa ghafla kugombea nafasi hiyo ya waziri mkuu kunahitimisha utawala ambao haukuingilika wa Barisan Nasional, BN, muungano ambao umeiongoza serikali ya Malaysia tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mnamo mwaka 1957. 

Mahathir amenukuliwa akisema hawana mpango wa kulipiza kisasi, dhidi ya serikali ya Najib, iliyokuwa imeelemewa na kashfa za ufisadi, bali wanataka kurejeshwa utawala wa sheria. Mahathir hapo awali aliapa kuanzisha uchunguzi dhidi ya kashfa hiyo ya ufisadi iwapo angechaguliwa, ili fedha hizo ziweze kurejeshwa nchini Malaysia.

Kulingana na Najib, kwa kuwa hakuna chama chochote kilichopata wingi wa viti unaotakiwa kwenye uchaguzi huo mfalme wa Malaysia atakuwa na jukumu la kumchagua waziri mkuu mpya, na kwamba National Front utaheshimu maamuzi yoyote yatakayofanywa na mfalme.

Amewataka Wamalaysia kuwa watulivu na kuwa na imani na hekima ya mfalme katika kumchagua kiongozi bora. 

Matokeo rasmi yanaonyesha muungano wa Mahathir wa Pakatan Harapan umeshinda viti 113 kati ya 222 vya bunge, hatua inayouwezesha kuongoza serikali. Muungano wa Najib, ulipata viti 76 pekee. 

Mahathir ameahidi kufanya upya makubaliano ya mikataba na China, pamoja na kubadilisha baadhi ya sera zilizotekelezwa na serikali ya Najib, ambazo ni pamoja na kodi za bidhaa na huduma, GST iliyoanzishwa na Najib katika kipindi cha siku 100 mamlakani, lakini pia kupitia upya sheria ya uwekezaji wa kigeni. 

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/APE/AFPE
Mhariri:Josephat Charo