SINGAPORE: Mkutano wa G7 kujadili biashara duniani
16 Septemba 2006Mawaziri wa fedha wa nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda-G7 wanakutana Singapore huku wasi wasi ukizidi kuhusu uchumi wa Marekani unaoonyesha ishara za kuzorota.Mawaziri hao kutoka Ujerumani, Uingereza,Ufaransa,Italia,Kanada,Japan na Marekani,wanatazamiwa kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kufufua majadiliano yanayohusika na biashara duniani.Waziri wa fedha wa Ujerumani, Peer Steinbrueck,alipozungumza kabla ya mkutano wa G7 mjini Singapore alisema,kuna hamu kubwa ya kuwa na makubaliano ya kibiashara kati ya pande mbali mbali.Hata hivyo,alikiri kuwa hadhani makubaliano yatapatikana hadi mwisho wa mwaka huu kuhusu majadiliano ya Doha kuhusika na biashara duniani.Majadiliano hayo yaliozinduliwa Doha nchini Qatar,Novemba mwaka 2001 yaliahirishwa mwezi wa Julai kwa sababu ya mgogoro wa Marekani na Ulaya kuhusu mageuzi ya kuwa na uhuru zaidi katika sekta ya kilimo.