1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Simba walioshirikishwa michezo ya sarakasi waokolewa

Admin.Lilian Mtono/AFPE29 Aprili 2016

Simba 33 waliookolewa katika vituo vya michezo ya sarakasi nchini Peru na Bolivia hatimaye wanarudishwa nchini Afrika Kusini, ambako watapatiwa matunzo maalumu, ikiwa ni pamoja na chakula na makazi.

https://p.dw.com/p/1IfM1
Afika hungriger Löwe
Picha: picture alliance/All Canada Photos/K. Lang

Hatua hiyo ya ureshwaji wa wanyama hao inatajwa na wanaharati wa kutetea haki za wanyama kuwa ni ubebwaji mkubwa zaidi wa wanyama hao wakubwa kwa kutumia usafiri wa anga.

Simba hao, wenye majina kama Zeus na Shakira, walihamishwa baada ya kuondolewa kwa sheria ya uhalali wa kutumia wanyama katika maonyesho hayo ya sarakasi nchini Peru, mwaka 2011 na Colombia mnamo mwaka 2013.

Wanapata usaidizi kutoka shirika la kimataifa la kuwalinda wanyama, ADI. Ni kweli inashangaza kuona simba wote hawa, baada ya kupata mateso na unyanyasaji kwa muda mrefu kwenye maonyesho hayo sasa wanarudishwa nyumbani Afrika, amesema rais wa ADI Jan Creamer.

Simba wote walipotoka huko walikuwa na matatizo ya kiafya, ambayo ni pamoja na minyoo na magonjwa mengine, aliongeza. Katika kipindi chao chote cha kuishi huko hawakupata chakula cha kutosha, kwa hivyo walikuwa na utapiamlo wa muda mrefu.

Gharama ya usafiri ni Dola 10,000 kwa kila Simba

Katika miezi ya hivi karibuni simba hao wamekuwa wakiishi wakiwa wamefungiwa kwenye makasha ya chuma yaliyopo katika eneo la wakimbizi Kaskazini mwa mji wa Lima, lakini wakiwa huko walikuwa wakilishwa vema na sasa wana afya njema, amesema Creamer.

Simba 24 waliookolewa kutoka Peru wataondolewa kutoka katika kituo cha dharura cha uokozi na kupelekwa uwanja wa ndege wa Lima, na baadae kuchukuliwa na ndege ya mizigo itakayokuwa na simba tisa waliookolewa kutoka Colombia.

Wazo ni kwamba simba atatoka kwenye kizimba na kuingia kwenye kizimba atakasafirishiwa - vizimba hivyo vimesanifiwa kurahisisha hilo na tunatumai kwamba kila kitu kitakwenda sawa.

Simba wengi walikuwa na matatizo ya kiafya
Simba wengi walikuwa na matatizo ya kiafyaPicha: picture alliance/AP Images/T. Mukwazhi

Kwa pamoja simba hao 33 watasafiri angani kwa masaa 15 hadi nchini Afrika Kusini, wakiwa kwenye maboksi maalumu ya kuwasafirishia wanyama ndani ya ndege hiyo iliyokodishwa na ADI. Wanatarajiwa kufika Jumamosi hii, ambapo watahifadhiwa kabla ya kupelekwa kwenye hifadhi ya simba iliyopo Emoya, Kaskazini mwa nchi hiyo, ifikapo mwezi October.

Simba hao watakuwa katika hifadhi yenye makazi yao asilia, na hii itakuwa mara yao ya kwanza katika maisha yao, amesema Creamer. Watatakiwa kuyatambua makazi hayo, kuna mazingira mazuri. ADI imesema usafirishaji huo ni mkubwa zaidi kwa wanyama wakubwa.

Simba hao wataanza maisha mapya baada ya mateso

Kwenye vikundi hivyo vya sarakasi, simba hao walikuwa wakilishwa vibaya na kubeba mizigo kuzunguka vizimba, ADI imesema. Kambi ya Colombia, ilikubali kuwatoa simba tisa, lakini iliwapasa polisi kutumia nguvu kuwatoa simba katika kambi ya Peru.

Karibu simba wote waliookolewa wamekatwa kucha, mmoja amepoteza jicho, na mwingine akiwa na uoni hafifu, na wengi wao wanaonakena kuwa na meno yaliyovunjika, na hivyo hawataweza kuishi kwenye hifadhi za wanyama, imesema ADI kwenye taarifa yake.

Kwenye makazi hayo mapya simba hao watafurahia eneo kubwa lililozungushiwa ukuta, ambalo pia lina mabwawa ya maji ya kunywa na mahali penye miinuko. Makazi hayo yatakuwa yakipanuliwa katika kipindi cha miezi ijayo wakati ambapo simba hao watakuwa wameyazoea mazingira na wao wenyewe kujuana.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Idd Ssessanga