1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silvio Berlusconi matatani ?

8 Oktoba 2009

Waziri mkuu wa Itali aahidi kujibu mashtaka mahkamani.

https://p.dw.com/p/K1vt
Berlusconi (hoi?)Picha: AP

HUKUMU DHIDI YA BERLUSCONI:

Waziri mkuu wa Itali Silvio Berlusconi, anakabiliwa na msukosuko tangu wa kisheria Mahkamani hata wa kisiasa madarakani: Hii inafuatia hukumu ya jana ya Mahkama Kuu ya Itali kubatilisha sheria inayomkinga waziri mkuu huyo asishtakiwe na hivyo, kufungua njia kwa yale mashtaka ya udanganyifu katika ulipaji-kodi na ya rushua dhidi yake kufunguliwa upya mjini Milan.Hatahivyo, waziri-mkuu Berlusconi, ametangaza kwamba, hatajiuzulu.

Hukumu ya jana ya Mahkama ya Itali ya kumvua waziri mkuu Silvio Berlusconi kinga ya kutoweza kushtakiwa,inaongezea juu ya orodha ndefu ya matatizo yanayomkabili Berlusconi.Pamoja na hayo, ni kashfa ya zina na makahaba iliohanikiza katika vichwa vya habari nchini Itali.Isitoshe, inatoa nafasi nyengine kwa washtaki wa serikali kudai waziri mkuu ahukumiwe.

Binafsi Berlusconi, ameendelea kuonesha ushupavu na kuapa kwamba, hatajiuzulu na ataendelea kutawala hata imara zaidi.Alisema ataonesha kwamba, mashtaka ya rushua dhidi yake ni ya kuchekesha.

JIBU LA BERLUSCONI:

"Kesi 2 dhidi yangu hazina msingi, ni za kuchekesha , za kipumbavu na nitabainisha hayo kwa wataliana mbele ya TV na nitajitetea mahkamani na kuwafanya wanaonituhumu kuonekana wapumbavu na kumuonesha kila mmoja wao ameumbwa kwa udongo gani na mimi kwa udongo upi ......iishi Itali, aishi maisha marefu Berlusconi."

Waziri mkuu huyo wa Itali, amewahi kumhujumu Rais wa nchi hiyo,sehemu kubwa ya vyombo vya habari,mahakimu na hata Mahkama ya Katiba iliomvua kinga kuwa eti inaelemea mrengo wa shoto na kupanga njama dhidi yake.

ONYO KWA UCHUMI:

Wachambuzi wa kisiasa, wameonya kuwa, mvutanio wa kisiasa unaotokana na hukumu ya jana ya Mahkama Kuu ya Itali, kunaweza kukaongoza kuitikisa Itali na kuathiri uchumi na shughuli Bungeni.

Wakati hakuoneshi kuna hatari ya kuitishwa uchaguzi na mapema nchini Itali, alao kwa hivi sasa, wahariri wamesema athari za hukumu ya jana na jibu la kifidhuli alilotoa Berlusconi, kumepalilia mvutano wa kisiasa kwa kadiri ambayo, haikuwahi kuonekana tangu kupita miaka mingi nchini Itali na kuutikisa uchumi wake.

Kwani, mawakili wa waziri mkuu huyo wamedai kwamba, hukumu ya jana itamshughulisha mno sana mahkamani na hivyo kulemaza shughuli zake za serikali.

ATHARI YA HATIA:

Hukumu yoyote itakayotolewa baadae na kumkuta na hatia,itakuwa pigo jengine la kumuaibisha waziri mkuu huyo.Hatahivyo, Berlusconi, hawezi kulazimishwa kujiuzulu kwa kadiri muungano wake wa vyama vya kihafidhina wenye wingi Bungeni,haukusambaratika.

Mwandishi:Ramadhan Ali /Rtr/afp

Mhariri:M.Abdul-Rahman