Silaha za Ujerumani zatumika vita vya Yemen - Ripoti ya DW
27 Februari 2019Kwa mujibu wa ugunduzi unaotokana na mradi wa utafiti uliopewa jina la #GermanArms, yaani silaha za Kijerumani, majeshi ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia yanatumia silaha na teknolojia ya Kijerumani kwenye operesheni zao za angani, ardhini na majini nchini Yemen.
Hata hivyo, akiulizwa na DW kwenye mkutano kuhusu usalama mjini Munich hivi karibuni, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Peter Altmaier, alisema yeye hafahamu chochote.
"Sijui chochote kuhusu silaha hizo. Kwenye serikali yetu ya muungano tumeweka wazi kwamba tunasitisha mara moja uuzaji na usafirishaji silaha kwa pande zinazohusika moja kwa moja na mzozo wa Yemen, na ambao sasa unatekelezwa. Hadi sasa sijasikia chochote kuhusu hilo," alisema waziri huyo anayetokea chama cha CDU cha Kansela Angela Merkel.
Ugunduzi wafichuwa
Licha ya wawakilishi wa serikali ya Ujerumani daima kukanusha kujuwa chochote juu ya kutumika silaha zilizotengenezwa Ujerumani kwenye vita vya Yemen, lakini timu ya watafiti wa DW ilichambua picha za vidio na satalaiti na kugundua mifumo kadhaa ya silaha zilizotengenezwa Ujerumani ndani ya Yemen, na hivyo kuthibitisha kuwa zinahusika kwenye mzozo huo.
Miongoni mwa mengine, uchunguzi huo ulibaini maeneo halisi ambayo yanapatikana magari kadhaa ya kijeshi ya Umoja wa Falme za Kiarabu ndani ya miji ya Aden na Al Khawkhah. Magari hayo yalikuwa yamebeba vituo vya silaha vya Fewas vilivyotengenezwa na kampuni ya silaha ya Ujerumani, Dynamit Nobel Defence - DND. Kwenye vidio ya mwezi Oktoba 2018, timu hiyo ilikitambua pia kifaru aina ya Lecrec cha Ufaransa kikiwa na mzinga aina ya Clara uliotengenezwa pia na DND.
Katika ugunduzi mwengine, mradi wa utafiti wa #GermanArms uligundua meli za kivita za Kijerumani zinazomilikiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu kwenye bandari ya Mokha nchini Yemen na ile Assab nchini Eritrea, ambacho ni kituo cha operesheni za vikwazo vya safari za baharini vinavyolengwa kundi la Wahouthi nchini Yemen.
Uchunguzi huo umeendeshwa kwa ushirikiano wa Deutsche Welle, Report München inayomilikiwa na kituo cha redio cha kusini mwa Ujerumani cha Bayerischer Rundfunk na jarida la Stern, pamoja na shirika la habari la kujitegemea nchini Uholanzi liitwalo Lighthouse Reports na mtandao wa uchunguzi wa Bellingcat.
Waandishi: Naomi Conrad/Nina Werkhäuser
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Yusuf Saumu