Siku ya pili ya kikao cha hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa
25 Septemba 2019Rais wa Iran Hassan Rowhani amepangiwa kuhutubia hadhara kuu , huku hotuba yake ikisubiriwa kwa hamu kubwa na viongozi wa kimataifa mnamo siku ya pili ya kikao cha hadhara kuu ya Umoja wa mataifa. Rowhani atahutubia mnamo wakati mivutano imezidi makali kati ya Iran na Marekani baada ya rais Donald Trump kuituhumu Iran kuwa muungaji mkono mkubwa wa ugaidi katika eneo la mashariki ya kati na kuahidi wakati huo huo kuzidisdha makali ya vikwazo dhidi ya Iran.
Rowhani anatarajiwa kujibu tuhuma alizotoa rais wa Marekani Trump mbele ya viongozi wa dunia na kufika hadi ya kuilaumu Iran kuhusika moja kwa moja na shambulio la hivi karibuni dhidi ya mtambo wa mafuta wa Saudi Arabia.
Kuna uvumi au pengine matumaini kwamba Trump na Rowhani huenda wakakutana pembezoni mwa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa ingawa rais Rowhani anashikilia irejeshwe kwanza hali ya kuaminiana kati ya pande hizo mbili.
Ni jukumu la Marekan i na Iran kuitumia fursa iliyojitokeza
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alizidisha juhudi zake za kuwatanabahisha viongozi hao wawili waketi katika meza ya majadiliano.Baada ya hotuba yake iliyodhihirika kukinzana na zile za msimamo mkali wa kizalendo za rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Brazil Jair Bolsonaro,rais Macron alisema kabla ya kuondoka New York " masharti ya kuitishwa haraka mazungumzo yamepatikana". Ni jukumu la Iran na Marekani kuidaka fursa hiyo" amesema.
Mbali na rais wa Ufaransa, kansela Angela Merkel wa Ujerumani, waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe nao pia wamezidisha juhudi za kuwatanabahisha rais wa Marekani na mwenzake wa Iran wakutane..Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan amesema ametumwa na rais wa Marekani apatanishe.
Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kuitisha mkutano mkubwa wa waandishi habari kabla hajaondoka New York kurejea Washington.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/dpa
Mhariri: Iddi ssessanga