Siku ya Kudumisha haki za binadamu
10 Desemba 2009Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuzikumbatia tofauti zetu ili tumalize ubaguzi.Wataalam wa Umoja wa Mataifa wameshauri kuwa kuna umuhimu wa kuziimarisha harakati za kuupiga vita ubaguzi hasa ikiwa azimio hilo limetimia miaka 60 tangu liidhinishwe.
Katika taarifa yake ya kuiadhimisha siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alitoa wito wa kuupiga vita vikali ubaguzi wa aina yoyote ile kote ulimwenguni,''Ubaguzi umelaaniwa vikali na mikataba yote ya kimataifa.Hata hivyo matamshi pekee hayatoshi.Lazima tupambane na ubaguzi na kutovumiliana kokote vinapodhihirika.''alisisitiza
Ibara 26 kati ya 30 za azimio hilo la kuupinga ubaguzi zinaanza na kauli zilizo na azma ya kuwaleta watu pamoja vilevile kuyafikiria maslahi ya wote.Kwa mujibu wa wataalam wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu juhudi zaidi zinahitajika ili kupambana na ubaguzi.Vita dhidi ya ubaguzi sharti viongezwe kasi yake na vipewe kipa umbele katika jamii zote. Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya haki za binadamu Navi Pillay alisisitiza kuwa ubaguzi hauna faida yoyote,''Ubaguzi unasababisha kutoaminiana,chuki,ghasia,uhalifu na hata ukosefu wa usalama…vilevile hauna faida zozote kiuchumi kwasababu unawapunguzia ari wahusika.Ubaguzi hauna manufaa yoyote katika jamii kwa kweli.''alifafanua
Wataalam wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa kuna umuhimu wa kuziheshimu tofauti za kidini,kitamaduni badala ya kuziona kama mambo ambayo yanautishia umoja wa jamii.Kwa sasa kuna mikataba mingi ya kimataifa iliyofikiwa kwa misingi ya kuupiga vita ubaguzi kwa mfano azimio la haki za watoto,haki za watu walio n ulemavu,haki za wakimbizi vilevile haki za wafanyakazi wahamiaji. Azma ya sheria hizi za kimataifa ni kuleta uwiano katika jamii mbalimbali.Hata hivyo ni mataifa machache ambayo yamefanikiwa kuzitimiza haki hizo.Hilo ni jambo la kufurahiwa kwani idadi ya wanaotendewa haki imeongezeka.Tofauti za mtu na mtu au jamii na jamii zina umuhimu mkubwa zaidi kwani zinachangia katika kuuimarisha uhusiano wa jamii.
Kamishna wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya haki za binadamu Navi Pillay alisisitiza kuwa tofauti katika jamii ni jambo muhimu na kila mmoja ana haki ya kukubalika katika jamii.''Kila mtu ana haki ya kutimiziwa haki zake zote.Hakuna anayepaswa kubaguliwa.Kuupiga vita ubaguzi ndio misingi yake kudumisha haki za binadamu.''alieleza
Baraza la Kutetea Haki za Binadamu lilianzishwa kwa minajili ya kuunga mkono heshima katika jamii ili kuzilinda haki zote za binadamu pamoja na uhuru wa wote.
Mwandishi:thelma Mwadzaya-UN Human Rights Council
Mhariri:Mohamed Abdulrahman