Siku ya kimataifa ya utoaji wa misaada ya kiutu
19 Agosti 2014Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha juhudi za utoaji wa misaada ya kiutu. Siku hii ni ya kulikumbuka shambulizi la bomu katika makao makuu ya Umoja ya Mataifa mjini Baghdad nchini Iraq mnamo Agosti 19 mwaka 2003 ambapo mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, raia wa Brazil, Sérgio Vieira de Mello na wenzake 21 waliuwawa.
Takwimu zinatisha. Mnamo mwaka 2003 shirika linaloshughulikia usalama wa wafanyakazi wa misaada, aidworkersecurity.org, liliorodhesha matukio 63 ambapo wafanyakazi 143 walitekwa nyara, kujeruhiwa au hata kuuwawa. Kufikia mwaka 2013 idadi ya mashambulizi imeongezeka kufikia 251 kukiwa na wahanga 460. Kutokana na takwimu hizi mashirika ya misaada, madogo kwa makubwa, yametoa onyo. Na hata Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya unataka kuuhamasisha ulimwengu kuhusu tatizo hilo na ndio maana Agosti 19 ikatangazwa siku ya kimataifa ya utoaji ya misaada ya kiutu.
Ripoti mpya kuhusu wafanyakazi wa utoaji misaada imechapishwa leo sambamba na siku ya kimataifa ya misaada ya kiutu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo wafanyakazi 155 wa kutoa misaada waliuwawa mwaka uliopita huku mashambulizi dhidi ya wafanyakazi hao yakiongezeka kwa asilimia 66 kote ulimwenguni, ikilinganishwa na mwaka 2012. Ripoti hiyo imeorodhesha mashambulizi 251 yaliyowaathiri wafanyakazi 460 wa kutoa misaada ya kiutu.
Ripoti hiyo iliyotayarishwa na shirika linalotoa ushauri la Humanitarian Outcomes, imeonyesha wafanyakazi 171 walijeruhiwa na 134 kutekwa nyara mwaka 2013. Mizozo inayozidi kutokota nchini Syria na Sudan Kusini imetajwa kama sababu kubwa ya kuongezeka kwa kasi mashambulizi, ingawa Afghanistan ndiyo nchi hatari zaidi ambako wafanyakazi 81 wa kutoa misaada waliuwawa mwaka uliopita.
Chuki dhidi ya vitu kutoka Magharibi
Profesa wa haki za kiraia wa chuo kikuu cha Ruhr mjini Bochum, Ujerumani, Hans Heintze, analaumu mabadiliko ya taswira ya vita kwa ongezeko la mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada. Akizungumza na DW profesa huyo amesema tangu mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani hakuna jeshi linaloweza kufaulu kirahisi katika vita vingi.
Mara kwa mara makundi ya kigaidi hufanya mashambulizi kwa nia ya kuvuruga utangamano na makundi ya wahalifu hushambulia misafara ya misaada. Lakini tatizo hasa ni tofauti kabisa, alisema profesa Heintze. "Pande zinazopigana vita kama wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu na magaidi huilinganisha misaada ya kiutu na fikra ya kimagharibi na hiyo huifanya kazi ya utoaji misaada kuwa ngumu mno."
Profesa Heintze ametoa mfano wa Afghanistan ambako shirika la msalaba mwekundu hutoa misaada akisema wapiganaji huliona kama shirika la mataifa ya magharibi na hivyo kulilenga katika mashambulizi yake, fikra ambayo si sahihi.
Ufyetuliaji risasi na utekaji nyara vimechangia karibu asilimia 50 ya mashambulizi na zaidi ya nusu yalifanyika wakati wafanyakazi wa misaada walipokuwa wakisafiri. Kwa mujibu wa takwimu za awali kufikia Agosti 13 wafanyakazi 79 wa misaada wameuwawa mwaka huu wa 2014. Wakati wa miezi ya Julai na Agosti, ongezeko la machafuko katika Ukanda wa Gaza na Sudan Kusini lilichangia sana ongezeko la mashambulizi ya wafanyakazi wa kutoa misaada.
Kampeni ya kuwalinda wafanyakazi mitandaoni
Mabango ya mwezi Agosti yametundikwa pamoja na kampeni katika mitandao ya kijamii imeanzishwa. Kupitia vitambulisho mbalimbali kama vile 'humanitarianheros', yaani mashujaa wa misaada ya kibinadamu, au 'ProtectOurVolunteers', yaani walinde wafanyakazi wetu wa kujitolea, watumiaji wengi wa mitandao hiyo wametoa miito ya kulindwa na kuheshimiwa wafanyakazi wa misaada, ambao katika mizozo yote hawaegemei upande wowote na badala yake husaidia pande zote.
Takwimu zinaonyesha ni wafanyakazi wa mashirika ya misaada kutoka maeneo husika wanaoshambuliwa au kutekwa nyara. Kinyume na hayo wafanyakazi wa kutoa misaada kutoka mataifa ya kigeni sio sana kujikuta katika njia panda. Mara nyingi wafanyakazi wa kigeni hushikilia nafasi za uongozi na ndio maana ni wachache katika mataifa kunakofanywa miradi ya utoaji misaada kuliko wenyeji wanaoyafanyia kazi mashirika hayo.
Hata miongoni mwa mashirika yenyewe ya misaada kuna tofauti. Mashirika madogo katika maeneo ya mikoani mbali na miji hushambuliwa kila mara kwa kuwa usalama unakuwa mbovu. Mapigano yanapochacha, mashirika makubwa kama Umoja wa Mataifa na Shirika la Msalaba Mwekundu hushambuliwa, hali ambayo inatakiwa kuugutusha ulimwengu wakati mashambulizi haya yanapotokea.
Mwandishi: Josephat Charo/Drechsel, Alexander
Mhariri: Iddi Ismail Sessanga