1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa ya haki za binadamu

10 Desemba 2010

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya haki za binaadamu, kiongozi wa shirika la Umoja wa mataifa la haki za binaadamu, Navi Pillay,amezitolea wito serikali mbali mbali duniani ziliowatia jela wanaharakati wa haki za binadamu

https://p.dw.com/p/QVFg
Kiongozi wa Shirika la UN la Haki za Binadamu Navanethem PillayPicha: AP

Tangazo lililosainiwa na kiongozi huyo wa Shirika la Umoja wa mataifa la haki za binaadamu, Bibi Navi Pillay, linazitaka serikali zilizowatia nguvuni wanaharakati wa haki za binaadamu kuwaachilia huru. Katika tangazo hilo, Bibi navi Pillay anasema kwamba kuwakosoa viongozi wa kisiasa kuhusiana na ukiukaji wa haki za binaadamu si kitendo cha uhalifu.

Bibi Navi Pillay pia amesema kwamba hatua kubwa imefikiwa katika kuheshimu haki za binaadamu mnamo kipindi cha miaka sitini iliyopita tangu kuanzishwa Jumuia ya Umoja wa mataifa. Akasema mamia kwa maelfu ya wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu katika kila pembe ya dunia, wamechangia kwa kiwango kikubwa ila'Baadhi ya nyakati tunausahau mchango wa watetezi walivyojitolea kupambana na dhuluma.waliubadili mkondo wa historia na wakafanikiwa kupambana na dhuluma na vitendo vya unyanyasaji kokote walikouona.Tunahitaji kuendelea kuzilinda haki hizo ili azma yao idumu,''alisisitiza.

 Navi Pillay alisema huu ni wakati wa kutoa shukrani za dhati kwa mashujaa hao, ambao wengi wao hawakujulikana nje ya mipaka ya nchi au maeneo walikoishi; na kuwakumbuka wale ambao leo hii wametupwa jela na serikali mbali mbali duniani. Akaendelea kusema kwamba huu ni wakati pia wa kufuatilia nini kitakachowafikia wale ambao wanazungumziwa sana katika vyombo vya habari.

Katika mkutano na waandishi wa habari leo asubuhi mjini Geneva, Bibi Navi Pillay alielezea wasiwasi wake kuhusiana na hali inayokabili makampuni ya tovuti yaliyoshirikiana na muanzilishi wa wikileaks, akisisitiza kua kinachotokea wakati huu ni majaribio ya kutaka kuzuia uhuru wa kusema. Amesema kwamba anaelewa kua hali inayojiri wakati huu kuhusiana na wikileaks ni mtihani mkubwa wa kutambua mipaka baina ya uhuru wa maoni na umuhimu wa kulinda usalama wa watu binafsi na wa taasisi za uongozi.

Kongo Oppositionspolitiker Floribert Chebeya Flash-Galerie
Marehemu Floribert Chebeya,mwenyekiti wa chama cha kutetea haki za binadamu,La Voix des sans Voix wa KongoPicha: picture-alliance/ dpa/dpaweb

Kiongozi huyo wa Shirika la Umoja wa mataifa la haki za binaadamu amesema kwamba katika nchi nyingi duniani bila kuzitaja nchi hizo, wanaharakati wa haki za binaadamu wanaendelea kusumbuliwa, kunyanyaswa na hata kukataliwa kabisa haki ya kuelezea maoni yao.

Alitoa tu mifano miwili, ikiwa ni pamoja na kuuwawa mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, marehemu Floribert Chebeya,  mwezi Juni uliopita pamoja na mwandishi habari wa Urusi, Anna Politkovskaia, alieuwawa mwaka wa 2006.

Mwandishi:   Gisimba, Jean-Francois/

Mhariri:  Miraji Othman