Siku ya haki za binadamu
10 Desemba 2007Lengo la kampeni hiyo ni kukumbusha juu ya masharti yaliyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja huu. Kauli kuu ya kampeni hiyo ni “Heshima na haki kwa sisi sote.”
Yaliyoandikwa chini ya kauli mbiu ni: Watu wote ni huru na wamezaliwa na heshima na haki sawa. Kwa maneno haya, shirika la Umoja wa Mataifa linataka kukumbusha juu ya makubaliano juu ya haki za binadamu ambayo yalitangazwa mnamo tarehe 10 Disemba mwaka wa 1948 kwenye mkutano mkuu na yaliyo na masharti 30. Makubaliano haya ni kama hali ya kufikirika ambayo bado haijafikiwa, lakini imekubaliwa na wananchi wote wanachama wa Umoja wa Mataifa kama msingi wa Umoja huu.
Bado tuko mbali na lengo hili, lakini angalau tumepiga hatua fulani. Pale, makubaliano haya kuhusu haki za binadamu yalipowekwa kama msingi wa uanachama, maana yake pia ni kwamba yanapaswa kutumika pia katika katiba za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Pia pale ambapo hadhi ya binadamu haiheshimiki, na vilevile katika nchi ambapo haki inategemea mamlaka, fedha au matakwa ya watu fulani kuliko mahakama inayojitegemea.
Makubaliano kuhusu haki za binadamu yameweka masharti kwa maisha ya pamoja katika dunia hii. Ni kama ahadi za serikali kwa wananchi wao pamoja na uhalalishaji wa kazi za watu wengi wanaopigania haki za binadamu ulimwenguni kote. Ikiwa ni kupigania usawa kati ya wanaume na wanawake, kudai haki ya elimu itekelezwe au kupinga mateso – wanaharakati wote wana msingi wa pamoja, yaani makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Inabidi kupinga vikali majaribio ya nchi fulani au makundi fulani kudhoofisha uhalali wa kimataifa wa haki za binadamu kutokana na tofauti za kitamaduni. Dunia hii inahitaji kuwa na maadili na malengo ya pamoja, hususa katika ulimwengu huu wa utandawazi. Tunahitaji maadili ya pamoja kwa mabara yote, dini, tamaduni na lugha zote.
Watu wote ni huru na wamezaliwa na heshima na haki sawa. Hata miaka sitini baada ya kuanzishwa, msingi huu bado ni halali.