1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali imeanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa.

Admin.WagnerD23 Novemba 2015

Mali leo(23.11.2015) imeanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kuwakumbuka wahanga wa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika kutokana na kuzingirwa hoteli ya kifarahari, yaliyowaua watu 19 kwenye mji mkuu, Bamako.

https://p.dw.com/p/1HAZv
Mali Radisson Blu Hotel in Bamako
Hoteli ya Radisson Blu mjini Bamako nchini MaliPicha: Reuters/J. Penney

Mataifa mengine ya jirani kama Senegal, Mauritania na Guinea zinaungana na taifa hilo kuonyesha mshikamano.

Uchunguzi wa kuwasaka waliohusika na mkasa huo bado unaendelea ambapo mpaka sasa hakuna utambuzi wa idadi wala utaifa wa wanaotuhumiwa kufanya shambulizi hilo ambalo limegharimu maisha ya watu 19, ambalo vilevile makundi mawili ya jihadi yamekiri kuhusika nalo.

Siku ya umwagikaji damu

Katika mkasa huo uliotokea Ijumaa watu waliokuwa na silaha waliizingira hoteli ya ya kifahari ya Radisson Blu, na kuwateka wafanyakazi na wageni wa hoteli 170. Shambulizi hilo lilifikia kikomo baada ya jeshi la Mali na vikosi vya kimataifa walishambulia jengo hilo, ambapo watu 19 waliuwawa, wakiwemo raia wa kigeni 14.

Waliouwawa katika mkasa huo ni pamoja na Warusi sita, Wachina watatu, Wabelgiji wawili, Mmarekani mmoja, Muisrael mmoja, Msenegali na idadi nyingine ya wanajeshi wa Mali.

Rais ya Senegal atoa pole

Rais wa Senegal, Macky Sall, jana Jumapili alitembelea mji wa Bamako kuonyesha mshikamano kwa Mali, mwanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS, ambayo kiongozi huyo ni mwenyekiti. Sall alisema Mali haitakuwa mpweke katika mapambano hayo, kwa sababu wote wanahusika.

Burkina Faso Senegals Präsident Macky Sall
Rais wa Macky Sall SenegalPicha: Reuters/J. Penney

Katika hatua nyingine jana Jumapili, wachunguzi nchini Mali inafuatilia kwa kina vyanzo mbalimbali vya uchunguzi wao kufuatia mauwaji hayo. Siku mbili baada ya mkasa huo ambao makundi ya Al Mourabitoun na al-Qaeda katika katika eneo la Afrika Magharibi yamedai kuhusika, kumekuwa na utambuzi duni wa waliofanya shambulizi.

Katika taarifa yake kitengo cha usalama wa taifa nchini Mali kimenukuliwa na katika televisheni ya nchi hiyo kikisema maeneo kadhaa yamekuwa yakifuatiliwa. Na kwamba hoteli iliyokuwa imeshambuliwa imekuwa ikifuatiliwa kwa uangalifu mkubwa.

Kwa kuzingatia siku ya operesheni ya kukabiliana na ugaidi katika hoteli hiyo Rais Ibrahim Bouba Keita alisema wote kwa pamoja wauwaji walifanikiwa kuuwawa katika eneo la hotel ingawa kulikuwa na taarifa nyingine za awali zilizosema kulikuwepo na mshambuliaji mwengine.

Ufaransa, ambalo lilikuwa lilikuwa likiitawala Mali katika enzi za ukoloni, linasaidia katika jitihada za sasa za uchunguzi na kwamba imetuma timu ya wataalamu katika kufanikisha jambo hilo.

Umwagikaji damu mjini Bamako ni miongoni mwa ishara za hivi karibuni kabisa kw kuzorota zaidi kwa hali ya usalama katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Wanamgambo wenye itikadi kali wenye kuungana na al-Qaeda walilidhibiti eneo la jangwa la kaskazini 2012 lakini mwaka mmoja baadae walitawanywa na operesheni ya kijeshi ya Ufaransa.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP/RTR
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman