Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Ujerumani azuru Marekani
2 Februari 2017Sigmar Gabriel atakua waziri wa kwanza wa mambo ya nje kukutana na waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson ambaye alithibitishwa rasmi katika wadhifa hao hapo jana.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema ziara yake hiyo inalenga kuwahakikishia washirika wao Marekani juu ya maslahi ya Ujerumani na kuwa anatarajia watakuwa na majadiliano mazuri na yaliyo wazi.
Ziara ya Gabriel inakuja ikiwa ni siku mbili baada ya mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu katika ikulu ya White House ambaye anatarajiwa kuongoza baraza la biashara la ikulu ya White House Peter Navarro kuishutumu Ujerumani kwa kutumia sarafu ya Euro kuikandamiza Marekani na washirika wake katika Umoja wa Ulaya.
Trump akosoa sera za Kansela Merkel kuhusiana na wahamiaji
Rais Donald Trump naye pia amemkosoa kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa sera yake ya kuweka milango wazi kwa wakimbizi huku pia Kansela Merkel akimshutumu Trump kwa kusaini agizo la kuwazuia wahamiaji kutoka mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu kuingia nchini Marekani.
Ilikuwa bado haijafahamika iwapo Sigmar Gabriel ambaye wiki iliyopita aliteuliwa kushika wadhifa huo wa waziri wa mambo ya nje pamoja na majukumu yake mengine kama Naibu Kansela wa Ujerumani, atakutana pia na Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence. Hata hivyo Sigmar Gabriel hakupangiwa ratiba ya kukutana na Rais Donald Trump.
Sigmar Gabriel amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa kufanya ziara hiyo mapema akisema Ujerumani ina maswali mengi kuhusiana na sera ya nje ya sasa ya Marekani.
Alisema kuna masuala muhimu katika ajenda ya kimataifa ambayo nchi hizo mbili pamoja na Ulaya kwa ujumla zinapaswa kushauriana kwa ukaribu zaidi ikiwa ni pamoja na ushiriki wa Marekani katika Jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi NATO.
Ujerumani tayari imeonekana kusitushwa na msimamo wa Donald Trump juu ya ushirikiano huo katika NATO. Hata hivyo serikali ya Ujerumani inatumaini kuwa waziri mpya wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson pamoja na waziri mpya wa ulinzi wa nchi hiyo James Mattis watamshauri vizuri Rais Trump.
Wakati Waziri wa ulinzi James Mattis akiwa tayari ameonesha msimamo wake wa kuunga mkono ushirikiano wa NATO waziri wa mpya wa mambo ya nje wa Marekani Tillerson amekuwa akikosolewa kutokana na ushirikiano wake na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakati waziri huyo alipokuwa mtendaji mkuu wa kampuni ya kimataifa ya mafuta na gesi ya Exxon Mobil.
Mwandishi: Isaac Gamba/DPAE/ECA
Mhariri : Iddi Ssessanga