Sierra Leone baada ya chaguzi za rais na bunge
17 Agosti 2007Kwa Benki Kuu ya Dunia,Sierra Leone tangu muda mrefu ni mfano wa mafanikio.Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka huu,kuhusu uongozi mzuri inasema, Sierra Leone sawa na jirani Liberia,ni miongoni mwa nchi zilizotia fora kupata maendeleo ya uongozi mzuri na ufanisi pamoja na kudhibiti upotovu na utulivu wa kisiasa.
Sasa,nchi kama Sierra Leone au Liberia zinaweza kutoa matumaini kwa bara zima la Afrika.Madola hayo ni ushahidi kuwa hata nchi zilizoteketezwa kwa vita na utawala wa mabavu,zinaweza kujitoa kutoka janga hilo,ilimradi kuna dhamira ya kisiasa.Kwa upande wa umma wa Sierra Leone, dhamira hiyo ya kisiasa ilidhihirika wakati wa chaguzi za mwisho wa juma lililopita:kwani chaguzi hizo zilikuwa huru na zilifanywa kihaki na kwa amani na wananchi wengi pia walijitokeza kupiga kura zao.
Atakaeshika wadhifa wa rais nchini humo, anangojewa na kazi ngumu kama vile kujenga upya taasisi za kiuchumi za nchi na kuvutia jumuiya ya kimataifa kwa azma ya kuleta amani katika taifa lililoshuhudia machafuko na kuchoshwa na vita.
Rais wa nchi jirani Liberia,Bibi Ellen Johnson-Sirleaf,ameonyesha kuwa changamoto kama hiyo inaweza kukabiliwa kwa mafanikio,kwa kuwa na msimamo mkali wa kisiasa tu.
Kwa kweli,kuna mengi yaliyofanana nchini Liberia na Sierra Leone:kwa mfano,katika nchi hizo mbili hakuna mfumo wa utawala,uchumi na sheria unaofanya kazi;theluthi mbili ya watoto na vijana hawawezi kusoma wala kuandika na asilimia 75 ya vijana hawana kazi.Vile vile daima upo uwezekano mkubwa wa machafuko kuzushwa na wanamgambo wa zamani wa makundi yaliyokuwa yakipigana.Wakati huo huo wanajeshi watoto walio wengi,wanataka kujumuishwa katika maisha ya kawaida.
Hakuna kinachoweza kutekelezwa kwa wakati ujao, pasipokuwepo usalama.Hayo,alitamka Bibi Johnson-Sirleaf baada ya kuchaguliwa kwake kama rais wa Liberia.
Sierra Leone,imeshachukua hatua ya kwanza kwa kufanya chaguzi za juma lililopita.Sasa jumuiya ya kimataifa ndio ina changamoto ya kuisaidia Sierra Leone kuwa na demokrasia iliyo tulivu pamoja na maendeleo ya kudumu.