Siasa zatawala vita vya corona, Congo
14 Aprili 2020Nchini Congo vita dhidi ya ugonjwa wa Corona vinaelelekea kuwa vita vya kisiasa, ambapo baada ya rais Felix Tshisekedi kutangaza hali ya dharura, maspika wa bunge na seneti wameitishwa kikao cha dharura cha bunge na seneti ilikujadili hatua hiyo ambayo wameitaja kuwa ukiukwaji wa katiba. Huku mvutano ukidhihirika baina ya bunge na ikulu, Korti ya katiba imempa haki rais kwa kuchukuwa hatua hiyo bila kulihusisha bunge.
Spika wa seneti Alexis Thambwe Mwamba na mwenzie wa Bunge Jeannine Mabunda wameitisha kikao cha dharura cha pamoja cha bunge na seneti ama congress ilikujadili hatua ya rais Tshisekedi ya kutangaza hali ya dharura ya kiafya nchini.
Kikao hicho kinatarajiwa kuitishwa kabla ya wiki hii kumalizika lakini tayari waziri wa mambo ya ndani ambae anatokea chama cha UDPS cha rais Tshisekedi amesema haitowezekana kuitishwa kikao hicho kwa sababu rais tayari katoa amri ya kutokuwepo na mikutano ya zaidi ya watu 20.
"Hatua ya kupiga marufuku mikutano inafuatia amri ya rais kutokana na kipindi hiki cha dharura, tunashangaa kuona kwamba maspika wa bunge na seneti wamepanga kuitisha kikao hivi sasa wakati ambapo wenyewe walitangaza kusitisha vikao vyote kutokana na ugonjwa wa Corona." alisema waziri huyo.
Soma Zaidi: Mikusanyiko ya mazishi marufuku DRC
Tarehe 15 Machi iliopita, kwenye sherehe ya kuzinduliwa kwa vikao vya bunge na seneti vya mwezi Machi, maspika hao wawili walielezea kwamba hakutokuwa na vikao vya bunge hadi hapo virusi vya corona vitakapopatiwa suluhisho. Wiki moja baadae rais Tshisekedi alitangaza hali ya dharura ya kiafya kote nchini. Lakini maspika hao wawili wamehisi kwamba rais alitakiwa kupewa kwanza idhini na bunge pamoja na seneti kabla ya kuchukuwa hatua hiyo.
Naibu spika wa bunge, Jean-Marc Kabund ambae anaongoza chama cha UDPS cha rais Tshisekedi ameelezea kwenye akaunti yake ya twitter kwamba kikao hicho ni njama ya kisiasa dhidi ya rais.
Jana Jumatatu rais Tshisekedi alitaka korti ya katiba kuelezea ikiwa hatua yake ilikiuka katiba au hapana. Kwenye uamuzi wake korti imelezea kwamba rais Tshisekedi hajakiuka katiba,lakini ikiwa muda wa hali ya dharura utaongezwa zaidi ya siku 30 ni lazima kuwepo na ridhaa ya bunge na seneti.
Mashirika ya kiraia yanaelezea masikitiko yake kutokana na mivutano ya kisiasa wakati ambapo raia wanasubiri kuona viongozi wakipambana vikamilifu dhidi ya ugonjwa wa Corona.
Katiba ya Congo inaelezea kwamba hali ya dharura inatangazwa na rais baada ya mashauriano na maspika wa bunge na seneti pamoja na waziri mkuu. Lakini Korti ya katiba inaelezea kwamba hata ya rais ilichukuliwa katika hali ya kipekee na kwa hiyo haija kiuka katiba.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo