1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za umaarufu Ulaya na USA zatishia haki za binadamu

Sylvia Mwehozi
13 Januari 2017

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rigths Watch limeonya katika ripoti yake ya mwaka huu kuhusu hali ya haki za binadamu duniani na kitisho cha siasa za umaarufu nchini Marekani na Ulaya.

https://p.dw.com/p/2VkUH
Kenneth Roth Human Rights Watch
Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Kuibuka kwa viongozi wanaotumia siasa za kutafuta umaarufu nchini Marekani na barani Ulaya na kunatishia ulinzi wa haki za msingi za binadamu huku viongozi hao wakihamasisha ukiukaji wa  haki na ukikteta duniani kote. 

Kuchaguliwa kwa Donald Trump kama rais wa Marekani baada ya kufanya kampeni iliyokuwa ikichochea chuki na  kutovumiliana na kuongezeka kwa ushawishi wa wa vyama vya siasa barani Ulaya ambavyo vinapinga haki kwa wote kumetajwa na Human Rights Watch kama kuuweka mfumo wa baada ya vita wa haki za binadamu katika hatari.

Wakati huo huo, viongozi walio na nguvu nchini Urusi, Uturuki, Ufilipino na China wamejimilikisha mamlaka mikononi mwao wenyewe badala ya kuwajibika kama serikali na kufuata utawala wa sheria, kama wadhamini wa ustawi na usalama.

Kongo Kinshasa Unruhen wegen Präsident Kabila
Kikosi cha kupambana na ghasia nchini DRC kikiondoa kizuizi barabarani Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Mwenenndo huu uliojaa operesheni za propaganda zinazokebehi viwango vya sheria na kudharau uchambuzi sahihi, moja kwa moja umeleta changamoto kwa taasisi za haki na sheria ambazo zimekuwa na kazi ya kuhamasisha utu, uvumilivu na usawa.

Siasa za Donald Trump

Katika ripoti ya kurasa 687 juu ya haki za binadamu duniani, shirika hilo limetathmini utekelezaji wa haki za binadamu katika nchi zaidi ya 90 na mkurugenzi wake Kenneth Roth anaandika kwamba kizazi kipya cha kimabavu kinataka kugeuza dhana ya ulinzi wa haki za binadamu. "Kuibuka kwa siasa za umaarufu ni kitisho kwa haki za binadamu, Trump na viongozi kadhaa barani Ulaya wanatafuta madaraka kupitia ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa watu wa mataifa ya nje, chuki kwa wanawake na sera za kuwalinda wazawa dhidi ya wahamiaji."

Mkurugenzi huyo anatolea mfano wa kampeni za Trump kama uhalisia wa siasa zilizokosa uvumilivu. Aliweka bayana mapendekezo ambayo yangeweza kudhuru mamilioni ya watu ikiwemo mipango ya kuwarejesha idadi kubwa ya wahamiaji, kuondokana na haki za wanawake, uhuru wa vyombo vya habari na mateso.

Ripoti hiyo inasema labda ikiwa Trump atabadilisha mapenekezo yake , lakini utawala wake unatoa kitisho cha kukiukwa kwa haki za binadamu.

Barani Ulaya hali ni hiyo hiyo, siasa za umaarufu zimelaumu mgawanyiko usio sawa wa kiuchumi kwa uhamiaji. Kampeni ya Brexit inatajwa kuwa mfano maarufu katika hili.

Vita ya Syria 

Syrien Interview Bashar al-Assad mit französischen Journalisten in Damaskus
Rais wa Syrai Bashar al-Assad anayetajwa kukandamiza haki za binadamu Picha: Reuters/Sana

Nchini Urusi Vladimir Putin aliitikia siasa hizo mwaka 2011 pamoja na ajena za ukandamizaji ikiwa ni vikwazo vingi juu ya uhuru wa kujieleza na kukusanyika, vikwazo kwa wakosoaji wa mitandaoni na sheria kali zinazozuia makundi huru. Nchini China kiongozi wa taifa hilo Xi Jinping hakushutuka kuhusu kushuka kwa ukuaji uchumi badala yake akaanzisha ukandamizaji mkali wa wapinzani tangu kipindi cha Tiananmen. "Hata leo, watu kama Rais Erdogan wa Uturuki, au Rais Sisi wa Misri kwa mara ya kwanza walikuwa na umaarufu mkubwa wakati Erdogan alienda kinyume na wanaodaiwa kupanga mapinduzi au Sisi alikwenda kinyume na chama cha udugu wa kiislamu. Lakini kila mmoja alikiuka haki za binadamu kwa kiwango kikubwa wakati walipozima maandamano yoyote ya amani dhidi ya utawala wao , " amesema Roth.

Nchini Syria Rais Bashar al-Assad aliyeungwa mkono na mataifa ya Urusi na Iran na Hezbollah aliweka mkakati wa vita na uhalifu wa kuwalenga raia katika maeneo yaliyokuwa yanashikiliwa na upinzani na kuvunja mahitaji ya msingi ya sheria ya vita.

Majeshi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS pia nayo yaliwashambulia raia na kuwanyonga watu walokuwa chini ya ulinzi wakati wakitekeleza mashambulizi ya raia duniani kote. Zaidi ya watu milioni tano walokimbia vita nchini humo wamekabiliana na ugumu katika kupata usalama.Jordan, Uturuki na Lebanon ambazo zinawahifadhi mamilioni ya wkaimbizi kutoka Syria zimefunga mipaka kwa wakimbizi wapya wanaowasili. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameshinwa kugawana jukumu la kuwapokea waomba hifadhi ama kutengeneza njia salama kwa ajili ya wakimbizi.

Barani Afrika 

Barani Afrika nako viongozi kadhaa wameongeza muda wa utawala, "mapinduzi ya kikatiba" ili kusalia madarakani wakati wengine wakitumia vurugu ili kukandamiza maandamano na  juu ya uchaguzi huru ama rushwa au utawala wa lazima.

Viongozi kadhaa barani Afrika pia waliikosoa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC na nchi tatu zikitangaza kujiondoa.

Ripoti hiyo inahitimisha kwa kusema mashambulizi haya yote ya kidunia yanapaswa kuangaliwa upya na serikali zitetee misingi na haki za binadamu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/HRW

Mhariri: Iddi Ssessanga