Siasa ya nje ya rais wa Marekani Donald Trump magazetini
30 Aprili 2018Tunaanzia Marekani ambako wahariri na walimwengu kwa jumla wanasubiri kujua kama rais Donald Trump "atayachana" au "ataamua yaendelezwe" makubaliano ya kimataifa kuhusu mradi wa nuklea wa Iran . Gazeti la "Mittelbayeriische Zeitung" linatupia jicho siasa ya nje ya rais wa Marekani Donald Trump na kuandika: "Mnamo wiki zinazokuja huenda rais Donald Trump akaachana na makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 kati ya Marekani, Urusi, China, Ufarasa, Uingereza na Ujerumani pamoja na Iran ili kuwazuwilia mamullah njia ya kutengeneza mabomu ya nuklea. Madhara ya uamuzi kama huo hayatakuwa na kifani. Madhara makubwa pia yanaweza kutokana na vita vya kibiashara ulimwenguni, kuzidi makali mzozo wa mashariki ya kati na kuitumbukiza katika hali ya mashaka jumuia ya kujihami ya NATO. Yote hayo lakini hayamtishi Trump. Anahisi shinikizo katika siasa yake ya nje ndiyo chanzo cha maendeleo yanayoshuhudiwa hivi sasa katika raasi ya Korea. Kwa hivyo anaishinikiza pia Iran "isicheze na Moto na Ghadhabu" na nchi za Ulaya anazitisha kwa mizinga ya ushuru."
Kilichomfanya Kim Jong Un abadilishe msimamo wake
Maoni sawa na hayo yameandikwa na mhariri wa gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" la mjini Halle anaesema:" Trump anaamini hasa hali katika raasi ya Korea ni matokeo ya siasa yake shupavu ya nje. Ingawa haijulikani bado sababu za aina gani za kiuchumi na malengo ya aina gani yamemfanya kiongozi wa Korea ya kaskazini abadilishe msimamo wake.Trump anaamini: Vitisho vyake ndio chanzo cha kubadilisha msimamo wake yule aliyekuwa akimwita " kikombora kifupi".
Msalaba katika majengo ya serikali Bavaria
Mjadala umeenea nchini Ujerumani kufuatia pendekezo la waziri mkuu wa jimbo la kusini la Bavaria, Markus Söder la kutundikwa misalaba katika majengo yote ya serikali katika jimbo hilo. Pendekezo hilo linakosolewa mpaka na viongozi wa kidini wanaohisi Söder anashindwa kutofautisha dini na siasa. Gazeti la "Passauer Neue Presse linaandika:" Ieleweke wazi kabisa kwamba kitambulisho cha Ukristo kina tafsiri za aina nyingi tu-miongoni mwa tafsiri hizo ni ile inayotokana na chimbuko la jadi la kikristo na kutoa picha ya mfumo huria wa kisiasa. Wakaazi wengi wa Bavaria wanauangalia msalaba kuwa ni sawa na kitambulisho cha nyumbani, wanauthamini zaidi kuliko sherehe za October au "Oktoberfest", au mavazi ya jadi ya jimbo hilo "Suruali za ngozi". Suala wanalojiuliza eti hayo yanatosha kutundika Msalaba katika majengo yote ya serikali? Waziri mkuu mchokozi Söder anasema "Ndio" na sauti zinazohanikiza zinaonyesha anazicheza vizuri karata zake. Seuze tena kampeni za uchaguzi zinakurubia."
Umuhimu wa May mosi
Mada yetu ya mwisho magazetini inatufanya tujiulize umuhimu wa may mosi, yaani siku ya wafanyakazi katika ulimwengu huu wa digitali. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Wengi wameanza kuusahau umuhimu wa may mosi, siku ya wafanyakazi na badala yake wanaitumia siku hiyo kama siku ya mapumziko tu. Ukweli lakini ni kwamba bidiii kwa masilahi ya kazi na masharti ya kazi yanayozingatia utu hayajapoteza umuhimu wake licha ya mfumo wa digitali."
Mwandishi:Hamidou/inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman