1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa na michezo ya kandanda ya Kombe la Dunia.

20 Juni 2006

Mnamo mwezi huu na ujao katika uwanja wa Olympic wa Berlin na viwanja vingine hapa nchini kunafanyika michuano ya kambumbu ya Kombe la Dunia, na watu wa mataifa mbali mbali, kutoka masafa ya karibu na mbali, wamekuja na kupokelewa na wenyeji wao wa Kijerumani kama marafiki.

https://p.dw.com/p/CHLS
Franz Beckenbauer, Rais wa tume ya maandalizi ya michezo ya Kombe la Dunia la kandanda, Ujerumani, mwaka 2006.
Franz Beckenbauer, Rais wa tume ya maandalizi ya michezo ya Kombe la Dunia la kandanda, Ujerumani, mwaka 2006.Picha: AP

Sasa Ujerumani ni nchi ya kidimokrasia na michezo ya Kombe la Dunia la kandanda, kinyume na ile ya Olympic, ni taabu kuitumia kwa sababu za kisiasa. Mwaka 1936 Ujerumani, chini ya utawala wa Wanazi, ilijitahidi kunyakua medali nyingi ili kudhihirisha nguvu za utawala huo. Pia wakati wa Vita Baridi, Marekani na Urussi zilishindana kuwa na medali nyingi, kila moja kuliko nyingine, kudhihirisha ubora wa mifumo yao ya utawala. Hali kama hiyo ya ushindani inaweza ikaonekana katika michezo ya Olympic ya mwaka 2008 huko Beijing, kati ya Marekani na Uchina.

Katika michuano haya ya kombe la dunia la kambumbu, japokuwa washabiki wa kutoka nchi mbali mbali za dunia zinazowania kombe hilo wamekuja na bendera zao za taifa na nyimbo za mataifa yao huimbiwa kabla ya kuanza michuano, hata hivyo, hakuna vita. Wachezaji hukumbatiana wanapofanyiana ngware, na unapomalizika mchezo hukumbatiana na kubadilishana flana zao, huku nyuso zao zikiwa na bashasha. Washabiki waliokosa tiketi za kuingia viwanjani huambulia na tafrija zilizosheni mabarabarani. Furaha juu ya furaha.

Zile hofu za mwanzo kwamba kunaweza kukatokea visa vya kibaguzi hazijatimia. Mwenyewe Rais wa Ujerumani aliyefungua michezo hiyo, alinukuliwa akisema:

+Nimepumua. Hata hivyo michezo yote haijamalizika na mtu anaweza kuona. Mimi nina hisia nzuri kwani imedhihirisha kwamba Wajerumani wanapenda na ni marafiki wa wageni. Kwamba wanaitendea urafiki na na kwa moyo wa furaha ule ule timu ya Togo kama wanavoitendea timu ya Uengereza au ya kutoka Marekani. Na kwa mimi hiyo inaonesha nchi hii iko wazi kwa dunia. Bila ya shaka, hiyo haina maana kwamba tunaweza au tunataka kufungia macho kwamba kweli kuna matatizo.+

Kweli dola kuu la kabumbu hivi sasa ni Brazil, ambayo imelichukua kombe hilo mara tano, ikiwa na washabiki hata katika zile nchi ambazo hushindana na nchi hiyo. Nchi za Kiafrika, licha ya kwamba hamna moja kati ya hizo iliowahi kulitwaa kombe hilo, hata hivyo ushabiki wa kandanda umetia fora huko. Ghana iliitwanga Jamhuri ya Cheki mabao mawili kwa bila, na rais wa nchi hiyo ya Kiafrika, John Kufuor, alikuja Ujerumani kujionea nchi yake ikilicharaza dimba. Alisema hivi alipofika Berlin kuonana pia na Rais wa Ujerumani, Horst Köhler…

+Tuna zaidi ya nchi 200 duniani, na ikiwa 32 tu ndizo zilizofikia katika michuano ya mwisho na nchi yako ni moja wapo, basi hapo unajua kwamba nchi yako ni miongoni mwa nchi zilizo bora kabisa. Hiyo inasaidia sana. Na zaidi ya hayo , kwamba tumeweza kuwemo katika tabaka lililo bora kabisa yaoneshe kwamba timu yetu ni thabití kabisa. Na mtu haendi kiwanjani kwa ajili ya tamasha tu. Tumekuja kikweli kutaka kulitwaa Kombe la Dunia.+

Uzuri ni kwamba kandanda ni mchezo wa tabaka zote, maskini na matajiri, weusi, weupe, na maji ya kunde, haujali tamaduni. Umoja wa Mataifa pamoja na bajeti yake kubwa inauoinea gere uongozi wa Shirika la Kabumbu Duniani, FIFA, linaloandaa michezo hii ya kila baada ya miaka minne. FIFA ina wanachama 207, ambapo Umoja wa Mataifa una wanachama 191 tu.

Katika risala yake mnamo siku ya ufunguzi ya michezo hiyo, Kofi Annan alisema angependa moyo huo wa ushindani uweko katika familia ya mataifa ya dunia, nchi zishindane, ijulikane ipi yenye kuheshimu kwa kiwango cha juu kabisa haki za binadamu, ipi yenye kuishinda nyingine katika kutokomeza vifo vya watoto wadogo, ipi yenye kutoa nafasi nyingi sana kwa watoto kwa ajili ya shule za sekondari. Ushindani wa aina hiyo pia ungeipeleka dunia yetu mbele zaidi.

Niliiangalia timu ya Ufaransa. Wengi wa wachezaji wake si Wafaransa wazawa, ni wahamiaji kutoka ngambo. Wachezaji hao wahamiaji wamekubalika katika nchi yao mpya. Lakini pia wamekua wachangiaji wa maendeleo katika nchi zao mpya na kuinyanyua juu ile hoja kwamba dunia yetu tunayoishi ni moja, tena ni kama kifuu, tukitaka tusitake lazima tuishi pamoja kwa amani…mustakbali wetu sote ni wa pamoja. Kweli, mataifa katika michguano hiyo huwania kupata magoli mengi kama iwezekanavyo, lakini Kofi Annan amesema goli lililo muhimu zaidi ni kuwa sehemu ya familia ya mataifa na watu mbali mbali.

Marekani, dola kuu ya kijeshi na kiuchumi, japokuwa imepiga hatua katika mchezo huo, lakini ina njia ndefu ya kupita kabla ya kufikiriwa kulitwaa kombe hilo. Kandanda ni mchezo unaohitaji ustadi na moyo wa ushirikiano katika timu. Fedha na ari ya serekali peke yake havitoshi. Timu ya Argentina kweli mwaka 1978 ilisaidiwa sana na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo kuwa washindi, lakini jambo hilo ni nadra kutokea. Leo hata Marekani na fedha zake zote, timu yake ya kabumubu haiwezi kuishinda ile ya Brazil. Na zaidi kandanda ni mchezo wa maajabu. Kila mtu aliduaa pale Senegal ilipoibwaga Ufaransa mwaka 2002, na Korea Kaskazini kuicharaza Italy mwaka 1966.

Mashabiki wengi wanasema Brazil italichjukua kombe tena, ikiwa ni mara ya sita. Wako wanaoitilia dau Argentina, Uengereza. Kuhusu mwenyeji, yaani Ujerumani, Franz Beckenbauer, kocha wa timu ya Ujerumani aliyeipatia ubingwa mwaka 1990 na sasa ni rais wa kamati ya maandalizi ya michezo hii, alisema:

+Sisi sio kati ya wale wanaotiliwa dau sana, lakini hiyo haina maana kwamba sisi au timu ya Ujerumani haiwezi kuwa bingwa wa dunia.+

Mwenyewe kocha wa timu ya Ujerumani, Jürgen Klinsmann, anahisi namna hivi:

+Karibu miaka miwili tumeijenga timu ambayo ina mambo mengi ndani yake, kwa upande wa mchezo, kimwili na kiakili imejitayarisha vuilivyo kwa ajili ya michezo hii. Hatuna woga kwa mpinzani. Tunajiamini kikweli.+

Itakapofika July 9, inatarajiwa watu bilioni moja, moja kwa sita ya wanadamu wote, watashuhudia finali, wakiwaangalia, hasa kupitia televisheni, watu 22 wakiufuatia mpira huku na kule ili kuidhihirishia dunia nani bingwa wa dunia. Kwa Wajerumani, pindi watashinda na kulitwaa kombe, basi itakua kilele cha mafanikio yao katika wakati huu, wakisahau matatizo yao ya kiuchumi na ukosefu mkubwa wa kazi, angalau kwa muda. Kwamba wamewapokea wageni, washabiki wa mpira milioni 4.5 nchini hapa, na mambo kwenda salama salimina, yote hayo yatahakikisha kwamba Wajerumani ni karibu wakamilifu katika kupanga na kuandaa.

Rais Köhler wa Ujerumani juu ya kandand, alisema hivi:

+Mimi mwenyewe napenda kabumbu. Nilipokuwa kijana na nilipokuwa katika jeshi, nilikua nacheza sana kandanda. Kwa hivyo ni jambo linalonigusa.+

Liishi kabumbu.