Shura Kitata na Brigid Kosgei washinda mbio, London Marathon
4 Oktoba 2020Brigid Kosgei alikamilisha mbio hizo kwa muda wa saa 2:18:01, mbele ya mshindani wake Mmarekani Sarah Hall aliyekimbia kwa muda wa saa 2:22:01.
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Bingwa wa Dunia upande wa wanawake Ruth Chepngetich kutoka Kenya aliyeshinda kwa muda wa saa 2:22:05.
Awali mbio za London Marathon zilipaswa zifanyike mwezi Aprili, lakini ziliahirishwa hadi mwezi Oktoba kufuatia janga la virusi vya corona.
Janga hilo pia limesababisha mashindano mengine muhimu duniani kuahirishwa mfano ikiwa ni Michezo ya Olimpiki ya Tokyo.
Shura Kitata wa Ethiopia ashinda kwa wanaume
Soma pia:Eliud Kipchoge aandika historia
Kwa upande wa wanaume Shura Kitata wa Ethiopia ameshinda mbio za Marathon za London na kumpiku bingwa mara nne wa mbio hizo Eliud Kipchoge kutoka Kenya aliyemaliza katika nafasi ya nane.
Kitata mwenye umri wa miaka 24 alithibitisha uwezo wake baada ya kushinda mbio hizo kwa muda wa saa 2:05.21, huo ukiwa ushindi wake mkubwa katika riadha.
Eliud Kipchoge ashindwa kutamba
Mkenya Vincent Kipchumba alishika nafasi ya pili, sekunde moja tu nyuma ya Kitata, huku nafasi ya tatu ikimuendea Muethiopia Sisai Lemma sekunde tatu nyuma ya Kipchumba.
Kipchoge ambaye pia ndiye bingwa mtetezi wa dunia katika mbio hizo, alipigiwa upatu kuibuka mshindi, hasa baada ya Kenenisa Bekele kujiondoa siku ya Ijumaa kufuatia jeraha. Hata hivyo bingwa huyo alimaliza katika nafasi ya nane.
(AFPE, RTRE)