Shule nchini Kenya kufunguliwa tena Januari 2021
7 Julai 2020Asilimia 90 ya wazazi nchini Kenya hawako tayari kuwarejesha watoto wao shuleni, idadi ya maambukizi ya COVID 19 inapoongezeka kupindukia. Kwa mara ya kwanza baada ya kuzozana kwa miezi kadhaa wadau katika sekta ya elimu nchini Kenya wamezungumza kwa sauti moja na kuridhia kutozifungua shule hadi Januari mwaka ujao. Akitoa tangazo hili waziri wa elimu Prof George Magoha ameelezea changamoto katika kuidhinisha masharti ya afya waliyowekwa na serikali kati ya wanfunzi.
Aidha, wasiwasi kuhusu baadhi ya waalimu waliozidi umri wa miaka 58 na wale walio na magonjwa sugu ni kigezo kilichozingatiwa, kuepuka kuyahatarisha maisha yao.
Hatua hii inamaanisha kuwa wanafunzi wote watabaki katika madarasa yao ya mwaka huu. Takriban watahiniwa milioni mbili wa shule za msingi na upili watafanya mtihani wao wa kitaifa mwaka ujao mwaka huu ukihesabiwa kama uliopotea kufuatia janga la COVID 19. Viongozi wamewataka wazazi sasa kuchukua jukumu lao kikamilifu kuhakikisha watoto wanasalia salama manyumbani.
Hata hivyo vyuo vikuu vimehimizwa kuendeleza masomo yake kupitia njia ya mtandao huku taasisi za kiufundi zikiruhusiwa kufungua mwezi septemba watakapozingatia masharti yaliyowekwa.
Wakio Mbogho, DW, Nakuru.