Shughuli za serikali ya Marekani zaanza kufungwa
1 Oktoba 2013Malaki ya watumishi wa serikali wanarudishwa nyumbani bila ya malipo na idara nyingi za serikali zimeambiwa zifunge milango. Sehemu kubwa ya shughuli za serikali ya Marekani zimefungwa kwa sababu serikali hiyo haina bajeti ya matumizi ya kawaida. Mgogoro huo maana yake ni kwamba wafanya kazi wa serikali kuu hadi milioni moja watapewa likizo bila ya malipo.
Baadhi ya huduma za umma kama vile miradi ya utafiti wa tiba zinazoendeshwa na idara za serikali pia zitasimama. Marekani imefikia hatua hiyo baada ya baraza la seneti linalodhibitiiwa na chama cha Rais Obama cha Demokratik kulikataa pendekezo la wajumbe wa chama cha Republican la kuusimamisha mpango wa huduma za afya wa Rais Obama.
Wabunge wa chama cha Republican wanaolidhibiti baraza la wawakilishi walitaka mchakato wa nipe nikupe na chama cha Demokratik. Wabunge wa Republican walikuwa tayari kuipitisha bajeti lakini kwa sharti la kuusimamisha mpango wa afya wa Obama ambao umeanza kutekelezwa leo.
Juu ya kufungwa kwa shughuli za serikali Rais Barack Obama amesema. "Kwa bahati mbaya bunge halikuutimiza wajibu wake." Hata hivyo baadhi ya wizara zitaendelea kufanya kazi kama vile ya ulinzi. Rais Obama aliwatumia wanajeshi ujumbe wa video kwa kusema. "Kama amirijeshi wenu nimehakikisha kwamba mtaendelea kuwa na uwezo, zana na yote mnayoyahitaji ili kuutekeleza wajibu wenu kwa taifa. Vitisho kwa taifa letu bado havijabadilika na hivyo tunawataka muwe tayari kwa dharura yoyote"
Kila upande unaulaumu mwingine kwa kushindwa kufikiwa kwa makubaliano. Rais obama ametahadhrisha juu ya madhara ya kiuchumi yanayoweza kutokea kufuatia kusimamishwa kwa shughuli za serikali. Amesema kasi ya ustawi wa uchumi inaweza kuvurugika.
Hatua iiyofikiwa leo pia inasababisha wasi wasi iwapo Marekani italifikia lengo lake hadi kati kati ya mwezi wa oktoba la kuongeza deni la serikali hadi dola Trilioni 16.7. Hisa barani barani Ulaya zimepanda juu kidogo mapema leo lakini wawekaji vitega uchumi wameingiwa wasi wasi.
Hata hivyo wachunguzi wanaamini kuwa wabunge wa Marekani watakaa chini pamoja haraka ili kutafuta ufumbuzi. Licha ya kuwa suala muhimu kwa masoko, madhali pana matumaini, masoko hayataathirika sana. Hayo ameyasema mtaalamu wa masuala ya fedha wa Unicredit mjini Munic, Christian Stocker. Wakati huo huo uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa chama cha Republican kitalaumiwa na wananchi wengi wa Marekani kwa kufungwa kwa shughuli za serikali.
Mwandishi: Mtullya Abdu. rtre,dpa,
Mhariri: Ssessanga Iddi