IFRC yatoa ombi la dharura ili kuwasaidia wakimbizi Congo
5 Juni 2024Shirikisho la kimataifa la mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, limetangaza ombi la dharura la dola milioni 57 ili kuwasaidia kwa haraka watu 500,000, wakimbizi wa ndani walio hatarini, pamoja na jamii zinazowakaribisha.
Mashirika hayo yameonya kuhusu "kuongezeka" kwa ghasia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, kwenye mpaka wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hitaji la dharura la kuwafikia wakimbizi
Shirika la Msalaba Mwekundu limesema mapigano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamesababisha mgogoro "mkubwa" ambao huenda usitambuliwe, na limeomba karibu dola milioni 60 kutoa msaada unaohitajika sana.
Soma pia: Umoja wa Afrika wakosoa jaribio la mapinduzi lililotokea DR Congo
Shirikisho la Kimataifa la mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC, mtandao mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani, umetahadharisha kuhusu "kuongezeka kwa kutisha" kwa vurugu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, kwenye mpaka wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa zaidi ya watu laki moja (100,000) walikimbia makaazi wiki iliyopita, wengi wao kutoka karibu na mji wa Kivu Kaskazini wa Nyanzale, ambako takriban watu 80,000 waliishi pamoja na makumi ya maelfu ambao tayari walikuwa wamekimbia mapigano ya awali katika eneo hilo.
Waasi wa M23 waliteka maeneo zaidi Alhamisi wiki iliyopita huku mapigano yakiendelea, na kuwalazimu watu wengine zaidi kuyakimbia makazi yao.
Shirikisho hilo linaleta pamoja zaidi ya wahisani milioni 16 duniani kote kusaidia watu walio hatarini, na walioathiriwa na majanga na dharura za kiafya.
Soma pia: Wakimbizi 3,000 DRC wajificha bondeni kufuatia mashambulizi
Athari zinazosababishwa na mapigano
Pierre Kremer, naibu mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa IFRC, ameuita "mgogoro wa kiwango kikubwa... ambao haujapewa tahadhari ya kimataifa kama inavyopaswa". Akizungumza kutoka Nairobi, Kenya, amesema, "watu wanaishi katika hali mbaya sana, wakiwa katika ukingo wa kuathirika kiakili, kimwili, na kifedha".
Beatrice Mitsa Tunisifu, ni mkimbizi wa ndani ambaye amepata hifadhi katika majengo ya shule ambako amekuwa akiishi na mtoto wake kwa miezi kadhaa baada ya kutoroka nyumbani kutokana na mapigano. "Maisha ni magumu sana kwa sababu ya njaa na magonjwa, " anaeleza.
Beatrice ni mmoja ya wanaofaidika na msaada wa chakula unaotolewa na shirika la msalaba mwekundu. "Wanafunzi wakirejea madarasani ni lazima tutoke nje. Wakati mwingine tunanyeshewa na hatuna pa kuenda. Mara nyingine tunabahatika kupata chakula mara moja kwa siku, ila wakati mwingine tunashinda na kulala bila kula."
Soma pia: Viongozi waungane kumaliza changamoto za demokrasia na usalama, Afrika.
Misaada mingi inawafikia wale walio katika kambi karibu na Goma, lakini inapungua kwa sababu ya mahitaji mengi ya watu, na kukosekana kwa ufadhili wa kutosha.
Pierre Kremer, anasema, "ombi lao litawezesha shirika la Msalaba Mwekundu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuongeza juhudi zao, kwa kutumia vifaa vilivyopo na miundo ya usaidizi kupanua ufikiaji wao kati ya familia zilizohamishwa na jamii zinazowapokea."