1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la ICRC lataka Mikataba ya Geneva iheshimiwe

Josephat Charo
30 Septemba 2024

Mikataba ya Geneva iliyoridhiwa 1949 kufuatia vita vya pili vya dunia inajumuisha dhamiri ya ubinadamu, maadili yanayovuka mipaka na dini.

https://p.dw.com/p/4lDUm
Mirjana Spoljaric, Mkuu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, ICRC.
Mirjana Spoljaric, Mkuu wa shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, ICRC.Picha: Peter Schneider/picture-alliance/KEYSTONE

Mkuu wa kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC Mirjana Spoljaric ametahadrisha juu ya kupuuzwa wazi wazi kwa mikataba ya Geneva katika mizozo kote ulimwenguni. Katika mahojiano na gazeti la kila siku la Uswisi Le Temps yaliyochapishwa jana Jumapili, Mirjana amezitaka nchi mbalimbali kwa haraka zijitolee tena kuheshimu sheria za kimataifa.

Alisema sheria ya kimataifa ya kibinadamu kwa utaratibu inakanyagwa na wale wanaoongoza operesheni za kijeshi. Ametaja idadi ya watu waliojeruhiwa na kuuliwa wakati wa migogoro ya Gaza, Sudan na Ukraine, ambayo amesema imepitiliza mawazo yao.

Mkuu huyo pia amesema ni lazima sasa kuchukua hatua kwa kuunga mkono sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ambayo kazi yake ni kupunguza athari za migogoro ya kivita na kuwalinda raia.

Ijumaa iliyopita kamati ya ICRC ilizindua mpango pamoja na nchi sita zikiwemo Brazil, China, Ufaransa, Jordan, Kazakhstan na Afrika Kusini, katika jitihada ya kuimarisha uungwaji mkono wa kisiasa kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.