1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la mpango wa chakula duniani lakanusha kwamba maafisa wa Ethiopia wanazuwia misaada kwenda Oagaden.

Mohammed Abdul-Rahman24 Julai 2007

Ni baada ya waasi kuutaka umoja wa mataifa ufanye uchunguzi juu ya madai hayo yaliotolewa na baadhi ya duru za kibalozi.

https://p.dw.com/p/CHAa
Moja wapo ya shughuli za usambazaji chakula za Shirika la mpango wa chakula dunian WFP barani Afrika.
Moja wapo ya shughuli za usambazaji chakula za Shirika la mpango wa chakula dunian WFP barani Afrika.Picha: WFP

Shirika la mpango wa chakula la umoja wa mataifa limesema,Serikali ya Ethiopia haizuwii misaada kufika katika mkoa wa mashariki, lakini vikwazo vya kibiashara pamoja na mafuriko ni mambo ambayo bado yanaweza kuzusha janga la kibinaadamu katika eneo hilo. Matamshi ya shirika hilo, yamekuja baada ya kundi la waasi linalojiita chama cha Ogaden ukombozi wa taifa kusema hali imefikia kiwango kinachohitaji zingatio la kimataifa.

Chama hicho Ogaden National Liberation Front cha wenye asili ya Kisomali katika Ethiopia, kimekua kikipigana ana serikali kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Matamshi yake kwamba hali ya chakula ni mbaya katika mkoa huo wa mashariki, yamekanushwa pia na maafisa wa Ethiopia. Msemaji wa Shirika la mpango wa chakula-World Food Programme katika mji mkuu wanchi jirani ya Kenya-Nairobi, amesema serikali haizuwii misaada inayokwenda Ogaden kwa sababu shirika hilo linasambaza misaada ya chakula katika sehemu tatu za mkoa huo, wakati limeanza pia kutathimini juu ya usambazaji katika sehemu tatu nyengine.

Lakini pamoja na hayo akasema shirika hilo na wafadhili wengine wanabakia kuwa na wasi wasi. Peter Smerdon pamoja na hayo akasema kwamba vizuizi vya biashara, nyendo za msaada kutokana na operesheni za kijeshi, pamoja nna mafuriko aya msimu, ongezeko la bei na sababu nyengine, ni mambo yanayoweza kusababisha janga la binaadamu miongoni mwa jamii.

Maafisa wa serikali ya Ethiopia hawakuweza kupatikana kuzungumzia suala hili na makala iliochapishwa na jarida la New York Times karibuni , ambapo kundi hilo la waasi katika mkoa huo unaopakana na Somalia lilidai uchunguzi wa umoja wa mataifa, baada ya gazeti hilo kuwakariri wanadiplomasia wa magharibi na maafisa wa shughuli za misaada wakiwashutumu maafisa wa Ethiopia kwa kuzuwia misaada.

Ogaden ni eneo lenye uhaba wa barabara na ambalo wakaazi wake wengi ni wafugaji ngamia wenye desturi ya kuhama hama, na ni shida kwa wanaharakati wa haki za binaadamu au waandishi habari kuwafikia

Mnamo mwezi uliopita, waziri mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi alitangaza hatua za kupambana na chama cha ukombozi wa Ogaden , waasi ambao wanasema wanapigania haki ya kujiamulia mambo yao wenyewe, ikiwa sehemu masikini kabisa nchini Ethiopia. Ethiopia inasema chama hicho ni kundi la kigaidi likisaidiwa na hasimu yake-Eritrea.

Kikijibu matamshi ya shirika la mpango wa chakula duniani kwamba maafisa wa Ethiopia hawazuwii misaada na kuwa shirika hilo linaendelea na shughuli zake katika sehemu tatu, chama cha ukombozi wa Ogaden kimesema misaada hiyo inasambazwa katika maeneo ambako hali ni shwari, na sio katika sehemu ambako mapigano yanaendelea, na ambako ndiko wanakoishi sehemu kubwa ya wakaazi.

Kwa upande mwengine hata hivyo Shirika hilo la umoja wa mataifa linasema harakati za kijeshi ziolizoanza mwezi Mei ziliapamba moto mnamo mwezi wa Juni na kuvuruga usambazaji wa misaada ya dharura. Lakini tani 2,200 za chakula sasa zimetumwa katika maeneo ya Ogaden ya Shinile, Afder na Liben ambako wakaguzi wa shirika hilo la mpango wa chakula wanahakikisha inawafikia wale wenye kuihitaji.

Taarifa ilisema chombo kingine cha misaada cha umoja wa mataifa OCHA kitaongoza ujumbe wa pamoja wa mashirika hayo kwenda Ogaden leo Jumatano, kukutana na maafisa wa sehemu hiyo pamoja na watu wengine.

Afisa Smerdon alisema ni muhimu kwani ucheleweshaji wowote utakua na athari kubwa kwa binaadamu kwa kuwa mkoa huo ulikumbwa na majanga ya ukame na mafuriko mwaka jana na ni karibuni tu umeanza kupata afuweni. Mafuriko zaidi huenda yakatokea Agosti au Septemba. Hadi usambazaji chakula ulipoanza mwezi huu, wengi wanaokabiliwa na njaa mkoani Ogaden walikua hawakupata msaada wowote wa chakula tangu mwezi Januari. Kutokana na hayo bei zimepanga na baadhi ya nyakati hata masoko huwa hayana kitu.