Shirika la Medicins Sans Frontieres - MSF lathibitisha mauaji ya wafanyakazi wake wawili Mogadishu
30 Desemba 2011Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo, wafanyakazi hao wawili waliouwawa jana ni Philippe Havet, mwenye umri wa mika 53, kutoka Ubelgiji, na Andria Karel Keiluhu, mwenye umri wa miaka 44 kutoka Indonesia.
Havet alitajwa kuwa mratibu mwenye ujuzi mwingi kuhusu maswala ya dharura, na alikuwa amelifanyia kazi shirika hilo la madaktari wasio na mipaka tangu mwaka 2000 katika maeneo kadhaa yenye ghasia, ikiwemo jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Lebanon na Sierra Leone. Keiluhu alikuwa daktari aliyelifanya kazi na shirika hilo tangu mwaka wa 1998 barani Asia na Afrika.
Shirika hilo la MSF limesema litawahamisha baadhi ya wafanyakazi wake kutoka Somalia kutokana na sababu za kiusalama, lakini litaendelea kutoa huduma zake na msaada wa kiutu mjini Mogadishu na kwingine nchini Somalia. Limeongeza kuwa limeshtushwa na kuhuzunishwa na kisa hicho cha jana cha mauaji. Kwa mujibu wa duru za polisi, afisa wa usalama alifyetua risasi ndani ya kiwanja cha ofisi za MSF. Sababu za tukio hilo bado hazijajulikana.
Miili ya watu hao wawili ilisafirishwa kutoka Somalia hadi Kenya hii leo pamoja na mfanyakazi mwingine wa kimataifa. Ufyatuaji huo wa risasi ndilo shambulio la hivi punde kufanywa dhidi ya maafisa wa misaada ya kiutu nchini Somalia, mojawapo ya sehemu hatari zaidi duniani kwa wafanyakazi wa misaada. Vikosi vya usalama vilimkamata mshukiwa huyo wa mauaji, ambaye mashahidi walisema ni mfanyakazi wa shirika hilo la MSF, raia wa Somalia.
Wiki iliyopita, mtu aliyejihami kwa bunduki aliwauwa wafanyakazi watatu wa misaada, raia wa Somalia, akiwemo mfanyakazi mmoja wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, katika eneo la kati la Hiran.
Katikati ya mwezi Oktoba, Wahispania wawili wanaofanya kazi na shirika la MSF walitekwa nyara na watu waliojihami katika kambi kubwa ya wakimbizi nchini Kenya, Daadab. Kambi hiyo imewakusanya wakimbizi wengi kutoka nchini Somalia ambao wameyakimbia machafuko nchini mwao. Shirika la Medicins sans Frontieres limetoa huduma nchini Somalia tangu mwaka wa 1991, wakati taifa hilo lilipotumbukia kwenye lindi la vita vinavyoendelea vya wenyewe kwa wenyewe.
Kwingineko msemaji wa jeshi la Kenya amesema kuwa wapiganaji watano kutoka kundi la wanagambo la alShabaab na mwanajeshi mmoja wa Kenya wamekufa kwenye makabiliano. Wanajeshi wa Kenya waliingia nshini Somalia kupambana na wanamgambo wa kundi hilo hatari. Wakati huo huo, kamati ya kimataifa ya shirika la msalaba mwekundu imesema imetuma vifaa vya dharura vya kimatibabu vinavyohitajika kusini mwa Somalia.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Miraji Othman