1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu, limeipongeza Libya kwa kuwaachia huruwauguzi wa kibulgaria na daktari wa kipalestina.

Mohammed AbdulRahman24 Julai 2007

Lakini linasema sasa Libya haina budi kurekebisha mfumo wake wa sheria.

https://p.dw.com/p/CB2W
Rais Parvanov wa Bulgaria ambaye amewasamehe wauguzi hao watano wa kibulgaria na daktari wa kipalestina.
Rais Parvanov wa Bulgaria ambaye amewasamehe wauguzi hao watano wa kibulgaria na daktari wa kipalestina.Picha: AP Photo

Wauguzi hao watano wa kibulgaria na daktari huyo wa kipalestina walisafirishwa leo hadi mji mkuu wa Bulgaria Sofia baada ya kupatikana maafikiano baina ya Libya na Ufaransa na umoja wa ulaya. Baada ya kuwasili wote sita wakasamehewa na rais Georgy Parvanov.

Akizungumzia hatua hiyo, mkurugenzi wa shirika la kimataifa la haki za binaadamu katika mashariki ya kati na Amerika kaskazini Malcolm Smart alisema maafisa wa Libya sasa hawana budi kuhakikisha kesi kama hiyo sasa haitokei tena, na kwamba wanapaswa kufanya mageuzi katika mfumo wa kisheria nchini humo, ili kisa kama hiki kisitokee.

Wauguzi na daktari huyo walikamatwa 1999 na kupatikana na hatia Mei 2004 kwa kuwaweka makusudi watoto 438 damu iliokua na virusi vya ukimwi katika hospitali ya Benghazi. Tangu wakati huo watoto 56 wamekufa. Hukumu ya kifo kwa wauguzi na daktari huyo ikabatilishwa kuwa kifungo cha maisha na kufikiwa makubaliano ya ulipaji fidia wa dola milioni moja kwa familia ya kila muathirika.

Wafungwa hao , wamedai hawakua na hatia na kuwa kuungama kwao makosa kulitokana na kuteswa.Mmoja wa wauguzi hao watano SNEZHANA DIMITROVA alikua na haya ya kusema juu ya kuachiwa huru.“Sijui niseme nini, Nilikua pia nikilisubiri tukio hilo, na sasa ninafuraha kwamba nilichokisubiri kimekuwa kweli .”

Wakati huo huo Umoja wa ulaya umeahidi kuinua daraja ya uhusiano wake wa kisiasa na kiuchumi pamoja na Libya, miongoni mwa matakwa yanayosemekana yalisisitizwa na Libya.

Rais wa halmashauri kuu ya ulaya Jose Manuel Bw Barosso aliipongeza Libya kwa kile alichokiita msimamo madhubuti na kwamba Umoja wa ulaya umejitolea kufanya kazi pamoja na libya kuelekea mustakbali wa pamoja wa pande hizo mbili.

Kwa upande mwengine Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye nchi yake ilishiriki katika mazungumnzo ya mwisho tangu Jumapili yaliosaidia kuachiwa huru wafungwa hao sita akiwemo kamishna wa ulaya wa mashauri ya kigeni Benita Ferrero Walnder na mkewe Sarkozy Cecilia Sarkozy, amethibitisha kwamba ataelekea Libya kesho kwa mazungumzo na kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mjini Sirte Alisema anataka kuisaidia Libya irudi katika jamii ya mataifa.

Rais Sarkozy atafuatana na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Bernard Kouchner. Rais huyo wa Ufaransa alisema si umoja wa ulaya wala Ufaransa ililioilipa fedha Libya lakini aliipongeza Qatar ambayo alisema imesaidia mno katika mawasiliano na Libya juu ya kisa cha wabulgaria hao.

Mjini Sofia balozi wa Marekani nchini Bulgaria John Beyrle akiikaribisha hatua hii ya Libya alisema Marekani itafanya kila iwezalo kutoa mchango katika kushughulikia maafa yaliowapata watoto wa Kilibya walioambukizwa virusi vya Ukimwi.