Shirika la IAEA latimiza miaka 50
29 Julai 2007Miaka iliyopita,shirika la IAEA,limegonga vichwa vya habari kila kulipozuka wasiwasi wa kuwepo majeribio ya kutengeneza silaha za nyuklia kinyume na sheria.Mara nyingi,habari hizo zilihusika na Irak,Iran na Korea ya Kaskazini.
Wajibu wa shirika la IAEA umetambuliwa na jumuiya ya kimataifa,ikiwa ni pamoja na hata nchi zinazokaguliwa na shirika hilo,hadi maafisa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo,Mohammed ElBaradei kutunukiwa Zawadi ya Nobel ya Amani katika mwaka 2005.
Historia ya IAEA yadhihirisha uhalali wa kusherehekea kuundwa kwake.Rais wa zamani wa Marekani,Dwight D.Eisenhower alipohotubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 8 Desemba mwaka 1953 alisema:
“Enzi ya atomiki imeendelea kwa kasi kubwa,hadi kuwa kila mkazi duniani,anapaswa angalao kufahamu umbali wa maendeleo hayo ambayo yana umuhimu mkubwa kwa kila mmoja.Ikiwa wakazi duniani wanataka kusaka amani kwa njia ya kutumia akili, basi ni dhahiri kuwa lazima wafahamu ukweli ulio muhimu kabisa kuhusu uhai wa leo.“
Miaka minane baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili na Marekani kutumia mabomu ya nyuklia katika miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan na vile vile Soviet Union ya zamani kufanya jaribio lake la kwanza la bomu la nyuklia,dunia nzima ilikuwa katika hali ya mashaka na kukabiliwa na mustakabali wenye hatari iliyopindukia kiasi.Kwani wakati huo,nguvu za mabomu ya nyuklia ziliongezekwa kwa mara 25 kulinganishwa na ilivyokuwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.
Katika kambi ya Magharibi, Marekani,Kanada na Uingereza zilikuwa na ujuzi wa kutengeneza silaha za nyuklia na upande mwingine,ilikuwepo Soviet Union.Mashindano kati ya mataifa mbali mbali kujikusanyia silaha,yalizusha wasiwasi.Wakati huo huo,ilidhihirika kuwa utafiti wa kinyuklia ukitumiwa kwa amani,unaweza pia kuleta mengi yaliyo mema.
Kwa hivyo,Eisenhower akazindua utaratibu wa kuendeleza na kutumia yalio mema katika utafiti wa nyuklia.Kuambatana na mpango huo,kuliundwa Shirika la Nishati ya Nyuklia IAEA chini ya Umoja wa Mataifa.Shirika hilo likapewa dhamana ya kupunguza nguvu za silaha za nyuklia,kuzuia usambazaji wa silaha hizo na pia kuhakikisha matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.
Miezi kumi baada ya Eisenhower kutoa hotuba yake katika Umoja wa Mataifa,nchi 81 ziliidhinisha sheria za IAEA na maafisa wa shirika hilo wakaanza kufanya kazi tarehe 29 Julai mwaka 1957 kwenye makao yake katika mji mkuu wa Austria, Vienna.
Mara nyingi,katika maamuzi ya IAEA,siasa hazipewi kipaumbele,mataifa mengine yanapohusika,kama ilivyokuwa kuhusu Irak,Korea ya Kaskazini au Iran.Katika mifano hiyo yote,ilidhihirika kuwa maoni ya IAEA na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, yalitofautiana na yale ya Washington.Ikulu ya Marekani katika kesi zote tatu ilitaka kuchukua hatua kali wakati IAEA lilipendelea zaidi kuwa na majadiliano,ukaguzi mpya na hasa subira zaidi.