Shirika la Human Rights Watch latoa ripoti kuhusu Angola
13 Aprili 2010Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch-HRW, limesema kuwa Serikali ya Angola haijachukua hatua za kutosha kupambana na rushwa na uongozi mbaya. Hayo yamo katika ripoti ya shirika hilo ambapo limesema pia ingawa nchi hiyo ina utajiri wa mafuta, lakini hauwanufaishi masiki wa nchi hiyo.
Ripoti hiyo ya kurasa 31 kwa jinala "Uwazi na uwajibikaji nchini Angola", inaelezea jinsi serikali ilivyochukua hatua za wastani tu kuboresha uwazi baada ya Shirika hilo la Human Rights Watch kufichua katika ripoti yake ya 2004 kwamba mabilioni ya dola yaliyotokana na mapato ya mauzo ya mafuta, zilikiuka benki kuu kinyume cha sheria na kutoweka bila ya maelezo yoyote.
Ufafanuzi katika ripoti hiyo unaelezea ushahidi uliopatikana kuhusu rushwa na usimamizi mbaya pamoja na kupendekeza kinachopaswa kufanywa.
Mkurugenzi wa Mpango wa Biashara na Haki za Binaadamu wa Shirika hilo, Arvind Ganesan, alisema kwamba serikali ya Angola inahitaji kuchukua hatua madhubuti kupambana na rushwa na usiri unaohujumu haki za Waangola. Akaongeza kwamba hilo ni taifa lenye utajiri lakini watu wake wanaishi katika umasikini. Akizungumzia juu ya utafiti wao, Bwana Ganesan alisema, Angola ni mtoaji mkubwa kabisa wa mafuta katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini mamilioni ya wananchi wake hawana huduma za kutosha za kijamii. Angola imeorodheshwa nafasi ya 143 kati ya nchi 182, kwenye tarakimu za Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP, panapohusika na maendeleo ya binaadamu. Katika orodha ya Shirika la kimataifa la kupambana na rushwa, ''Transpareny International 2009," Angola iko nafasi ya 162 kati ya nchi 180, baada ya kuwa nafasi ya 158 mwaka 2008, ikiwa na maana rushwa inazidi kukithiri.
Ripoti hiyo pia ushahidi wa Dr Aguinaldo Jaime aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Angola kuanzia 1999 mpaka 2002. Kama ilivyoorodheshwa katika ripoti ya baraza la Seneti la Marekani Februari mwaka huu, Jaime anataja juu ya mlolongo wa matukio yenye kutia shaka shaka, ya uvushaji wa dola milioni 50 hadi kwenye mabenki ya Marekani. Katika kila tukio Benki husika ama ilikataa kuzipokea fedha zilizotumwa au kuzirudisha muda mfupi baada ya kutumwa. Katika kipindi cha miaka mitatu aliyokua gavana, serikali haikuweza kuorodhesha dola bilioni 2 na milioni 4 zimekwenda wapi.
Taarifa za hivi karibuni za Rais Jose Eduardo dos Santos, yaelekea kuonyesha utayari wa serikali katika kupambana na rushwa. Ametamka juu ya sera ya kutomvumilia yeyote. Aidha, wakati baraza la Seneti la Marekani, likifanya utafiti wake hivi karibuni kuhusiana na rushwa nchini Angola na kwengineko, kiongozi huyo wa Angola akatangaza sheria mpya ikiwa na lengo la kukabiliana na rushwa ndani ya serikali. Hata hivyo, kwa kuwa rais huyo na chama chake tawala cha MPLA wako madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kikiwemo kipindi chote ambapo rushwa ilikidhiri bila kiasi. Human Rights Watch linasema, wenye shaka shaka watakuwa wakisubiri kuona hatua madhubuti zinachukuliwa.
Zaidi ya hayo, katiba mpya imepitishwa hivi karibuni ikimpa mamlaka Rais Dos Santos kubakia madarakani kwa miaka 13 zaidi. Tayari ameshatawala kwa miaka 30. Wadadisi wanasema kama kweli Angola inataka kupamabana na rushwa, basi hatua anazolenga Rais dos Santos hazina budi zitekelezwe kivitendo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (Human Rights Wathch Report)
Mhariri: Abdul-Rahman