1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la Human Rights Watch laitaka Zimbabwe kukomesha machafuko

Josephat Nyiro Charo29 Septemba 2010

Mikutano 13 ya hadhara ya kukusanya maoni ya umma kuhusu katiba mpya imeahirishwa katika mji mkuu Harare kufuatia machafuko hayo

https://p.dw.com/p/PQ04
Rais wa Zimbabwe, Robert MugabePicha: AP

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch Jumatatu wiki hii (28.09.2010) limeonya dhidi ya mashambulio yanayofanywa na wafuasi wa rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, wakati nchi hiyo ikiendelea na juhudi za kutafuta katiba mpya.

Shirika hilo limesema ongezeko la machafuko nchini Zimbabwe wakati wa mikutano ya kijamii kabla kufanyika kura ya maoni kuhusu katiba mpya na kutiwa mbaroni kwa wanaharakati wa makundi ya kijamii kunaashiria ukosefu wa mafanikio katika juhudi za kukomesha ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo. Shirika hilo pia linasema matukio hayo yanaonyesha kuwa Zimbabwe imeshindwa kutekeleza mageuzi ya sheria za haki za binadamu yanayohitajika kwa haraka nchini humo.

Serikali ya umoja wa kitaifa ya Zimbabwe ilianzisha mfululizo wa mikutano ya kijamii mwezi Juni mwaka huu kwa lengo la kukusanya maoni ya raia kuhusu katiba mpya. Mikutano hiyo imegubikwa na machafuko yanayozidi kuongezeka na vitisho vinavyotolewa na wafuasi wa chama cha Zimbabwe African National Union - Patriotic Front, ZANU-PF na askari wa zamani waliopigania ukombozi wenye mafungamano na chama hicho. Katika siku chache zilizopita, machafuko yameendelea kuwa mabaya, huku mikutano hiyo ikiwa imefikia katika mji mkuu Harare na mji wa Bulawayo. Kutokana na machafuko hayo, mikutano 13 iliahirishwa mjini Harare.

Chama cha ZANU-PF na washirika wake kinaendelea kufanya mateso bila kuwa na hofu ya kuadhibiwa na polisi hawachukui hatua yoyote, amesema Rona Peligal, mkurugenzi wa Afrika wa shirika la Human Rights Watch. Peligal ameongeza kusema, "Serikali ya Zimbabwe inahitaji kukomesha mashambulio hayo na iruhusu mikutano ya kukusanya maoni ya umma kuhusu katiba iendelee bila machafuko."

Shirika la Human Rights Watch limeihimiza serikali ya Zimbabwe kuchukua hatua za haraka kukomesha mateso na kuunda mifumo muafaka ya sheria na uchaguzi kuhakikisha chaguzi zinafanyika kwa njia huru, haki na halali, kwa mujibu wa mkataba ulioiunda serikali ya umoja wa kitaifa kati ya chama cha ZANU-PF na chama cha Movement for Democtatic Change, MDC. Serikali inatakiwa pia ibatilishe au ifanyie mageuzi sheria zote kandamizi kama vile sheria ya utangamano wa raia na usalama na sheria kuhusu uhalifu, ambazo zinaibana haki ya kuandamana. Polisi wameitumia sheria kuhusu usalama kuwatia mbaroni wanaharakati wa makundi ya kijamii.

Serikali pia inatakiwa iheshimu na itilie maanani mageuzi mapya ya kisheria kuhusu haki za binadamu yaliyojumuishwa kwenye katiba ya sasa, hususan yale yanayowataka maafisa wa serikali kuheshimu utawala wa sheria na kuhakikisha kuna uhuru wa kushiriki kwenye shughuli za kisiasa nchini Zimbabwe.

Shirika la Human Rights Watch lilipokea taarifa kuhusu machafuko katika miji ya Harare, Bulawayo, Masvingo, Mashonaland Magharibi na Mashonaland Mashariki wakati wa mikutano ya kukusanya maoni ya umma kuhusu katiba mpya. Inaripotiwa mashambulio yalifanywa na maafisa na wafuasi wa chama cha ZANU-PF dhidi ya wanavijiji wanaofahamika kuwa wafuasi wa chama cha MDC, pamoja na wanaharakati wa makundi ya kijamii wanaosimamia na kuangalia mchakato mzima wa kukusanya maoni ya raia.

Shirika hilo limesema waliofanya machafuko hayo wanatakiwa wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria na watetezi wa haki za binadamu wanaozuiliwa baada ya kuripoti mashambulio yaliyofanywa na chama cha ZANU-PF wanapaswa kufutiwa mashtaka yanayowakabili. Amesema machafuko na ukandamizaji hauna manufaa kwa mchakato mzima kuelekea kura ya maoni iliyopangwa kufanywa mwaka ujao. Bila mageuzi ya sheria kuhusu haki na kuwajibika kwa ukiukaji unaoendelea, machafuko yaliyoikumba Zimbabwe mwaka 2008 huenda yakatokea tena.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/hrw.org

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman