1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la HRW lazungumzia mgogoro wa Sudan Kusini

Mjahida27 Februari 2014

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema uhalifu wa kivita umetekelezwa na pande zote hasimu katika mgogoro wa Sudan Kusini, huku likiripoti visa vya ukatili katika wiki kadhaa za ghasia.

https://p.dw.com/p/1BGL5
Ghasia za Sudan Kusini
Ghasia za Sudan KusiniPicha: Reuters

Maelfu ya watu wameuwawa huku zaidi ya watu 900,000 wakiachwa bila makao katika mapigano ya zaidi ya miezi miwili, kati ya waasi na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na wanajeshi kutoka nchi jirani ya Uganda.

Ripoti hiyo ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema wanajeshi kutoka pande zote mbili, wametekeleza wizi na kuharibu mali ya raia ikiwemo vifaa vya kutoa misaada ya kibinaadamu, inayohitajika kwa wingi, kuwalenga raia, na kutekeleza mauaji ya kikabila.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo katika eneo la Afrika Daniel Bekele amesema visa vya ghasia dhidi ya raia ni vya kushtusha na kwamba pande zote zinapaswa kusimamisha dhuluma hiyo. Bekele ameuomba Umoja wa Afrika uzingatie kuanzisha mara moja uchunguzi wake ulioahidi siku nyingi ya mauaji ya raia wa Sudan Kusini.

Baadhi ya waasi
Baadhi ya waasiPicha: Reuters

Katika mji wa Bentiu, moja ya miji ilioathirika zaidi na mapigano katika nchi hiyo inayozalisha mafuta, Waasi wanasemekana kupekua masoko na mashirika ya misaada wakati walipokuwa wanaudhibiti mji huo, na kabla ya wanajeshi wa serikali kuutwaa mji, waasi walitekeleza visa vya wizi kabla ya kuanza kuwaua kwa kuwapiga risasi raia wa eneo hilo.

Lakini hata baada ya wakaazi wengi kutoroka mapigano katika mji wa Bentiu baada ya serikali kuudhibiti kikamilifu mji huo, wanajeshi wake pia waliwapiga risasi na kuwauwa raia waliobakia, lilisema shirika hilo la Human Rights Watch.

Bado watu wanayakimbia mapigano

Kwa upande mwengine maelfu ya watu bado wamekusanyika katika majengo ya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, wakihofia mapigano zaidi kati ya wanajeshi wa Rais Salva Kirr anayetokea kabila la Dinka, na wale wa makamu wa rais wa zamani Riek Machar anayetokea kabila la Nuer. Ghasia nchini humo zilianza Desemba 15 mwaka jana wakati rais Salva Kiir alipomshutumu Riek Machar kupanga njama za kutaka kumpindua.

Mazungumzo ya kutafuta amani yanayofanyika nchini Ethiopia yamekwama huku makubaliano yaliotiwa saini tarehe 23 Januari na pande zote mbili ya kusimamisha mapigano yalikiukwa kutokana na ghasia zinazoendelea.

Mazungumzo hayo yamekwama kutokana na waasi kukataa kutia saini makubaliano ya mahali pa kuwaweka waangalizi wa kuhakikisha makubaliano ya kusimamisha mapigano yanafuatwa. Hata hivyo juhudi za kutafuta amani bado zinaendelezwa mjini Addis Ababa Ethiopia.

Wakaazi wakikimbia mapigano
Wakaazi wakikimbia mapiganoPicha: Phil Moore/AFP/Getty Images

Wakati huo huo wataalamu waliwaambia wabunge wa marekani kwamba rais Barrack Obama anapaswa kuchukua juhudi zaidi za kusimamisha visa vya ghasia Sudan Kusini na jirani yake Sudan.

JohnPrendergast, Mkurugenzi wa zamani wa Afrika katika baraza la kitaifa la Usalama wakati wa utawala wa rais wa zamani Bill Clinton, alisema jana kwamba wakati ni sasa wa kuleta juhudi za kupatikana kwa demokrasia na utengamano katika eneo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman