1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo zaidi zatolewa Rais Mugabe kung'atuka madarakani

Sekione Kitojo8 Desemba 2008

Rais Robert Mugabe atakiwa kuondoka madaraka.Umoja wa ulaya wapania kmwekea Rais Mugabe vikwazo zaidi.

https://p.dw.com/p/GBo3
Akina mama wakitoka kuchota maji kutoka katika mashimo na mifereji nchini Zimbabwe.Picha: AP

Shinikizo zaidi zimeendelea kutolewa kumtaka rais wa zimbabwe Robert Mugabe kung'atuka madarakani kufuatia kuzorota kwa hali nchini humo. Umoja wa Ulaya unapania kumwekea Rais Mugabe vikwazo katika hatua za kwanza za kumshinikiza aondoke madarakani. Rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy ni miongoni mwa viongozi ambao wameongezea sauti zao kuhusiana na Rais Mugabe.



Katika mkutano na wanahabari mjini Brussels Ubelgiji mkuu wa sera za mambo ya nje wa umoja wa ulaya Javier Solana amesema la muhimu hivi sasa ni kutia shinikizo za kisiasa dhidi ya Rais Mugabe ili kumwondoa madarakani.


Matamshi ya solana yanawadia huku vyombo vya habari vya serikali nchini Zimbabwe, vikishtumu mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kutokana na vikwazo utawala wa rais Mugabe ulivyowekewa na mataifa ya Ulaya. Ugonjwa huo kufikia sasa umesababisha vifo vya karibu watu 600.


Zimbabwe imekabiliwa na mvutano wa kisiasa tangu uchaguzi wa mwezi marchi mwaka huu ambao yadaiwa rais Mugabe alishindwa na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai. Kiongozi huyo wa upinzani kisha alijiondoa katika raundi ya pili ya uchaguzi huo na hivyo kumfanya Mugabe kupata ushindi wa moja kwa moja.


Makubaliano ya kugawana madaraka kati ya Rais Mugabe na Tsvangirai yalitiwa saini mjini Harare tarehe 15 mwezi September, lakini hadi sasa hayatekelezwa kufuatia mvutano wa kugawana wizara umuhimu.


Waziri wa maswala ya nje wa Uingereza David Milliband amesema ni muhimu kutafuta njia za kuhakikisha sauti za wazimbabwe zinasikika, akisisitiza kuwa walieleza msimamo wao katika uchaguzi uliofanyika mwezi Marchi mwaka huu. Uingereza imekuwa ikichukua msimamo mkali dhidi ya Zimbabwe kwa muda mrefu.


Waziri Mkuu wa uingereza Gordon Brown alikuwa kiongozi pekee wa umoja wa ulaya kususia mkutano wa umoja wa ulaya kwa mataifa ya afrika mwezi december mwaka jana, kutokana na kuwepo kwa rais Mugabe. Na hivi Leo Waziri huyo mkuu alikuwa na haya ya kusema

"hali hiyo haiwezi kuendelea ,na nadhani ulimwengu mzima unasema imetosha,hili ni janga la kiutu, ni kuvunjika kwa jamii, ni utawala uliomwaga damu, na ambao haujawatendea haki watu wake."


Baadhi ya mawaziri wa mashauri ya kigeni kutokana umoja wa ulaya waliofanya mkutano wao hivi leo mjini Brusssels hawakuta kuzungumzía kwa undani swala hilo la Zimbabwe.


Waziri wa mashauri ya kigeni wa Luxermbourg Jean Asselborn amesisitiza kuwa umoja wa ulaya uko mbali sana na Zimbabwe na rais Mugabe kutoa shinikizo, akisema Jumuiya ya maendeleo kwa mataifa ya kusini mwa afrika –SADC imo katika nafasi nzuri kufanya hivyo.


Waziri wa maswala ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner ambaye taifa lake linashikilia urais wa umoja wa ulaya,hakutaja uwezekano wa kumwondoa Rais Mugabe madarakani.

Hata hivyo ametaka kuchukuliwa kwa hatua za dharura kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.


Zimbabwe imeishtumu uingereza kwa kutumia matatizo yaliyoko sasa,na pia kulipuka kwa ugonjwa wa kipindupindu kutafuta kuungwa mkono na mataifa ya magharibi kuivamia Zimbabwe.

Waziri wa maswala ya kigeni wa Bostwana,waziri mkuu wa kenya raiala odinga na askofu mkuu wa afrika kusini Desmond Tutu ni miongoni mwa viongozi kutoka Afrika wametaka rais Mugabe aondolewe madarakani. Rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy pia alijiunga na jamii ya kimataifa kumtaka Mugabe kuondoka afisini.






►◄