1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo zaidi laikumba Guinea.

Halima Nyanza22 Oktoba 2009

Utawala wa kijeshi nchini Guinea, unaendelea kupata shinikizo la Kimataifa, kutokana na mzozo wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/KCe8
Kiongozi wa kijeshi wa Guinea kapteni Moussa Dadis Camara. anazidi kuandamwa ajiuzulu.Picha: AP

Mbinyo zaidi unaendelea kutolewa na Jumuiya ya Kimataifa dhidi ya Guinea, baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono Uchunguzi wa mauaji ya watu wengi waliouawa nchini humo, huku Umoja wa Ulaya nao ukipitisha uamuzi wa kuiwekea vikwazo vya silaha nchi hiyo.

Kwa upande wake, Guinea nayo imeahidi kushirikiana na Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na mauaji hayo.

Waziri Mkuu wa Guinea Kabine Komara ameahidi kuunga mkono Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na mauaji hayo ya raia yaliyofanywa na jeshi la nchi hiyo.

Amesema wameuthibitishia kwa barua, Umoja wa Mataifa azma yao ya kuunga mkono Tume hiyo ya kimataifa kuchunguza mauaji hayo.

Amefafanua kwamba iwapo watashindwa kutoa ushirikiano kwa tume hiyo watashutumiwa kwa kujaribu kuficha ukweli.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya siasa, Haile Menkerious aliitembelea Guinea mwishoni mwa wiki iliyopita na mapema Jumatatu ya wiki hii kukutana na maafisa wa utawala wa kijeshi wa nchi hiyo akiwemo kiongozi wa utawala huo, kapteni Moussa Dadis Camara na Waziri Mkuu Kabine Komara.

Awali kiongozi huyo wa Utawala wa Kijeshi nchini Guinea aliunda Tume huru ya uchunguzi yenye wajumbe 31, kuchunguza mauaji hayo na kwamba itafanya kazi kwa kushirikiana na Tume ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa.

Wakati Umoja wa Mataifa ikiunda tume ya uchunguzi, Baraza la Usalama la umoja huo, limeunga mkono uchunguzi huo dhidi ya mauaji ya watu wapatao 150 waliouawa baada ya wanajeshi kuufyatulia risasi umati wa watu waliokuwa wakihudhuria mkutano wa upinzani katika mji mkuu wa nchi hiyo Conakry.

Balozi wa Ufaransa Gerard Araud, nchi ambayo ina kura ya turufu katika baraza hilo, amesema Waafrika lazima wawe wengi katika tume hiyo, ambayo pia inapaswa kuwajumuisha wanawake kwa sababu vitendo vya udhalilishaji dhidi yao pia vimedaiwa kutokea wakati wa ghasia hizo.

Nao Umoja wa Ulaya umesema utaiwekea vikwazo vya silaha Guinea kufuatia mauaji hayo ya waandamanaji waliokuwa wakiipinga serikali.

Uamuzi huo unatarajiwa kupitishwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa umoja huo katika mkutano utakaofanyika Jumatatu na Jumanne ya wiki ijayo mjini Luxembourg.

Hatua hizo zote zimeelezwa kwamba zitaongeza shinikizo la kimataifa kumtaka kiongozi huyo wa kijeshi kujiuzulu.

Vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya vitahusisha pia kuzuia fedha na vikwazo vya kusafiri barani Ulaya.

Jumuiya ya kimataifa inazidi kuiwekea vikwazo Guinea tangu Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika magharibi, ECOWAS, ilipotoa wito huo kama anavyosema Katibu Mtendaji wa ECOWAS Dokta Mohammed Ibn Chambas.

Marekani na Umoja wa Ulaya zimemtaka kiongozi wa kijeshi nchini Guinea ajiuzulu, huku Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ikichunguza mauaji hayo ya watu wengi yaliyotokea katika nchi hiyo ambayo inaongoza duniani kwa kusafirisha nje madini ya asili yanayotumiwa kutengenezea aluminium.

Kapteni Moussa Dadis Camara aliiingia madarakani baada ya mapinduzi ya Desemba mwaka jana, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Lansana Conte.

Mwandishi: Halima Nyanza (dpa, Reuters,afp)

Mhariri: Josephat Charo