Shinikizo linazidi dhidi ya Gaddafi
1 Machi 2011Muammar Gaddafi anapuuza shinikizo la kimataifa.Mnamo siku ya 14 ya kilio cha wapenda mageuzi,Muammar Gaddafi na vikosi vyake wanadhibiti mji mkuu Tripoli tuu na jimbo lake.Kwa mujibu wa kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia nishati,Gunther Oettinger,visima muhimu vya mafuta tayari vinadhibitiwa na makundi ya kikabila na vikosi vilivyonyakua maeneo hayo.
Upande wa upinzani unazungumzia uwezekano wa kuanza haraka kusafirishwa mafuta kupitia eneo la mashariki wanalolidhibiti.
Jumuia ya kimataifa inasaka njia za kumaliza mtafaruku nchini Libya na kufikiria hata uwezekano wa kutangaza eneo marufuku kwa ndege za Libya.
Jeshi la Marekani linaweka wanamaji na wanaanga katika maeneo ya karibu na Libya-hayo ni kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon iliyosema wataalam wanadurusu njia tofauti.Senetor John McCain anasema:
"Marubani wa Libya hawataweza kuruka ,kukiwa na eneo marufuku kwa safari za ndege."
Hata hivyo yadhihirika kana kwamba jumuia ya kimataifa haina msimamo mmoja kuhusu kutumiwa nguvu za kijeshi kumng'owa madarakani Gaddafi.
Baada ya Umoja wa Mataifa na Marekani,Umoja wa Ulaya pia umeamua kuuwekea vikwazao vya silaha Libya paamoja na kuzuwia mali ya viongozi wa Libya nchi za nje.Marekani imezuwia dala bilioni 30 tangu vikwazo hivyo vilipotangazwa.
Licha ya shinikizo lote hilo,Gaddafi anakataa kuregeza kamba.
"Wananchi wangu wananipenda-wako tayari kufa ili kunihami amesema Gaddafi katika mahojiano pamoja na kituo cha televisheni cha ABC.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Susan Rice ameyataja matamshi hayo ya gaddafi kuwa ni ya mtu mwenye "kuweweseka."
Nchi za Magharibi zinajiandaa kuusaidia upande wa upinzani uliounda baraza huru la taifa kushughulikia miji "iliyokombolewa."
Mbali na eneo la mashariki upande wa upinzani unadai kudhibiti miji kadhaa karibu na mji mkuu na katika eneo la magharibi,ikiwa ni pamoja na Nalout na Zawiyah.
Miji muhimu ya Misrata,ulioko mashariki na Gherian ulioko kusini inasemekana pia kudhibitiwea na upande wa upinzani.
Lakini jana usiku,vikosi vya Muammar Gaddafi vinasemekana vimefyetua risasi huko Mesrata na kuwaauwa watu wawili.
Mjini Tripoli vituo vya ulinzi vimewekwa katika eneo linalouzunguka mji huo mkuu ambako mkate na mafuta yanaanza kuwa haba.
Wakati huo huo rais wa Venezuela Hugo Chavez amezungumzia haja ya kuundwa tume ya kimataifa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya.
Mwandishi:Hamidou/Reuters,AFP
Mhariri: Abdul-rahman Mohammed