1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo laongezeka dhidi ya mapadre juu ya visa vya ngono

19 Februari 2019

Wahanga wa visa vya kingono walivyofanyiwa na mapadre wa kanisa Katoliki, wameunda muungano mpya wa kimataifa unaolenga kulishinikiza kanisa hilo kukabiliana na uhalifu huo, kufuatia miaka kadhaa ya mapambano.

https://p.dw.com/p/3Ddw1
Vatikanstadt - Messe zur Heiligsprechung im Vatikan von Paul VI und Oscar Romero | Papst Franziskus
Picha: Getty Images/AFP/F. Monteforte

Wahanga wa visa vya kingono walivyofanyiwa na mapadre wa kanisa Katoliki, wameunda muungano mpya wa kimataifa unaolenga kulishinikiza kanisa hilo kukabiliana na uhalifu huo. Hatua hii inafuatia miaka kadhaa ya mapambano waliyoyafanya wenyewe na wengine wakitafuta usaidizi kutoka kwa mashirika ya utetezi kwenye mataifa yao dhidi ya visa hivyo ndani ya Kanisa Katoliki. 

"Mimi ni Denise Buchanan, ninatokea Jamaica. Nilikutana na askofu Kenneth Richards na padre ambao walinibaka na kunipa ujauzito. Ingawa padre huyo alikiri kufanya tendo hilo, lakini bado yuko ndani ya kanisa."

Denise Buchanan ni mmoja wa wahanga na mwanachama wa muungano huo, unaotambulika kama Kumaliza Unyanyasaji wa Mapadri ama Ending Clerical Abuse (ECA), alipozungumza mbele ya waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi.

ECA inawaleta pamoja mamia ya wanaharakati kutoka mataifa mbalimbali watakaokusanyika mjini Rome wiki hii, wakati kiongozi wa kanisa Katoliki, Papa Francis atakapoongoza mkutano wa kilele wa maaskofu unaosubiriwa kwa hamu unaolenga kuzungumzia kuhusu kukabiliana na wimbi la kashfa za unyanyasaji wa kingono linalolitikisa kanisa hilo la Kikristo.

Chile | Fernando Karadima
Padri Fernando Karadima ni miongoni mwa mapadri waliowahi kutuhumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono nchini Chile.Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/L. Hidalgo

Mmoja wa waasisi wenza wa muungano huo Peter Sanders ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, huo ni mkakati wa dhati na wa kihistoria wa kimataifa, wa kuziunganisha sauti kutoka kona mbalimbali duniani na kuwa zenye mwito mmoja.

Kisa cha Saunders ni miongoni mwa vingine lukuki visovyohesabika vya wahanga wa unyanyasaji wa kingono ambao wamekusanyika pamoja na kuunda kundi hilo la ECA mwezi Juni iliyopita, ikiwa ni pamoja na wengine kutoka Chile, Poland, Uswisi, Ufaransa, Italia, Jamhuri ya Kidemokrasia wa Kongo na mataifa mengine.

Sanders amesema alinyanyaswa akiwa na miaka saba na mtu kutoka ndani ya familia yake, lakini pia alinyanyaswa na mapadre wawili akiwa sekondari, na wakati huo akiwa na miaka 12. Padre huyo pia alimlenga kaka yake aliyekuwa akisoma naye, na aliyemzidi miaka sita.

Chile Treffen der chilenischen Bischöfe in Punta de Tralca
Picha ya msalaba iliyopigwa nchini Chile. Kanisa Katoliki nchini humo limekabiliwa pia na mkururo wa kashfa za ngono kutoka kwa viongozi wa kanisa hilo. Picha: Getty Images/AFP/C. Reyes

Anasema, kanisa limekuwa likikataa kubadilika kwa miaka mingi, na kwa mtizamo wake anadhani hatimaye baada ya muda huo mrefu limeanza kukubali, kufuatia shinikizo linalotolewa na wahanga, vyombo vya habari vinavyoshirikiana na ECA duninani kote na hata maoni ya umma.

Malengo ya muungano huo, ni pamoja na kulishinikiza kanisa kuchukua mtizamo wa kutovumilia kabisa vitendo vya tamaa za kingono kwa watoto na kuwasaidia waathirika katika maeneo ambayo hawawezi kuzungumza, ikiwa ni pamoja na nchi zilizopo Afrika na Asia.

Akizungumza kuelekea mkutano huo wa kilele, mkurugenzi mwenza wa taasisi ya uwajibikaji wa maaskofu, ya BishopAccountability.org Anne Barret Doyle amelalama kuhusu kutokuwepo kwa mafungamano kati ya taarifa kali iliyotolewa na maaskofu kuhusu visa hivyo, ikilinganishwa na hatua zinazochukuliwa. Taasisi hiyo pia inashiriki mkutano huo.

Papa Francis amekuwa akishutumiwa kwa kutoonyesha utayari wa kumaliza vitendo hivi ndani ya kanisa kufuatia matamshi yake aliyowahi kuyatoa huko nyuma. Maaskofu wa Marekani mnamo mwezi November walifanya mkutano wao wa mwaka mjini Baltimore na walionyesha utayari wa kutekeleza mabadiliko ya wastani, lakini Vatican iliingilia mchakato huo katika hatua za mwisho na kuwataka kuachana na hatua hiyo.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef