Shida za kufikia suluhu miongoni mwa wakaazi wa Mosul
10 Agosti 2018Wanamgambo wa dola la kiislam IS walifanikiwa kuuteka mji wa Mosul walipokuwa wakisonga mbele nchini Syria na Iraq mnamo msimu wa kiangazi mwaka 2014, kwasababu walikuwa wakisaidiwa na mashabiki wao katika nchi hizo. Maelefu ya vijana wa Iraq walijiunga na kundi hilo la itikadi kali, wengi wao wakitokea katika eneo pana la Mosul. Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu mji huo ulipokombolewa na vikosi vya Iraq. Raia walioyapa kisogo kisogo maskani yao wanaanza kurejea nyumbani kujenga m aisha mepya. Lakini vipi wahanga na wahalifu wanaweza kuishi pamoja hivi sasa?
Ahmed Mohammed Abdulrahman ni meya wa Hammam Manqush, magharibi mwa Mosul. Ni sehemu ya mji mkongwe ulioteketezwa kwa vita - eneo la mwisho kudhibitiwa na wanamgambo wa dola la kiislam. Mapigano ya kuwania mji huo yameshamalizika lakini Abdulrahman anasema wakaazi wa mji huo hawana msimamo wa aina moja:"Tatiizo la IS litadumu miaka 100 zaidi. Watoto wa familia za IS na watoto wa familia nyengine wanapigana mtindo mmoja. Bila ya sababu. Wanapigana tu. Na wanalaumiana kila wakati. Kila wakati ambapo familia zaidi za IS watataka kurejea nyumbani ndipo na sisi tutakapozidi kukabiliana na matatizo".
Mji wote umeteketea isipokuwa msikiti wa kijani
Hamam Manquish ni karibu na msikiti wa Al Nuri uliopigwa mabomu. Akiwa huko ndiko Abu Bakr al Baghdadi, mkuu wa kundi la dola la kiislam alikotangaza utawala wake wa kikatili "Khalifa" juni mwaka 2014. Hivi sasa maeneo yote mawili, msikiti na Hamam Manqush yamesalia magofu . Lakini msikiti mkuu wa rangi ya kijani haujaathirika hata kidogo-wenyewe wanazungumzia kuhusu miujiza. Kabla ya vita familia 400 zilikuwa zikiishi katika eneo hilo. Nusu kati yao wakiwaunga mkono IS. Meya Abdulrahman na familia yake walibakia hadi mwisho wa mapigano.
Mwaka mmoja baada ya mji huo kukombolewa, familia 75 zimesharejea. Kuna hali ya kutoaminiana kutoka pande zote mbili. Hakuna anaekubali kutamka familia yake ilikuwa ikiwaunga mkoni IS. Hata hivyo familia zilizoathirika na kupoteza walio wao zimeghadhabika na zinawatafuta wa kulaumiwa.
Upinzani dhidi yakurejea nyumbani wafuasi wa IS
Omar Mohsin amempoteza mtoto wake wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 9. Hujuma ya mabomu im eangamaiza fam ilia ya kakaake pia. "Haiwezekani.Hawastahiki kuruhusiwa kurejea. Watoto wetu wote wamekufa. Sasa wanataka kurejea wao. Haiwezekani."
Mama mmoja anasema: "Mtoto wangu wa kiume na watoto wake walikuwa kama mauwa. Wamekosa nini? Wote wameteketezwa. Walikosa nini?
Kwa wastani kuna familia tatu zinazopanga kurejea nyumbani kwa wiki. Kila mmoja anaandikishwa. Lengo ni kuwafichua wanamgambo wa zamani waliojificha na watumishi waliokuwa wakisimamia utawala wa dola la kiislam. Familia 20 hivi za Hamam Manqush zinatuhumiwa kushirikiana na IS.
Meya wa mji huo Abdulrahman ana hakika suluhu haitowezekana bila ya waasisi na wasaidizi wao kupatikana.
Mpango wa suluhu ya taifa unahitajika
Naram Mohamad ni mwanafunzi wa sayansi ya komputa, mwenye umri wa miaka 24. Anasema anakumbuka jinsi mji wa Mosul ulivyokuwa ukivutia. Babaake alikuwa na duka. Naram anaamini ili suluhu iweze kupatikana mengi yanabidi kufanywa.
Majumba ya mawe unaweza kujenga upya kama unataka, na kama una pesa. Lakini kwa wakati huu tulio nao tunahitaji kuzijenga upya nyoyo zetu. Tunahitaji kuzifikia nyoyo za watu na kujifunza namna ya kufikiri kwa njia iliyo huru. Lengo ni kujenga upya nyoyo zetu. Hilo ndilo funzo tulilolipata baada ya miaka mitatu ya enzi za IS. Tunahitaji kujenga mazingira mepya Mosul,Tunabidi tubadilishe desturi zetu tunabidi tubadilishe msimamo wetu kuelekea wengine, tunabidi tubadilishe yale yote yaliyotufanya tufikie hapa tulipo."
Mtaalam huyo wa sayansi ya computa anatoa wito wa kubuniwa mpango jumla wa suluhu ya taifa.
Mwandishi:Sandra Petersmann/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Josephat Charo