1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria ya usalama wa China kwa Hong Kong yazusha wasiwasi

John Juma Mhariri: Sekione Kitojo
28 Mei 2020

Uingereza, Japan, Canada, Australia na Marekani zimeelezea wasiwasi wao kuhusu sheria ya usalama wa China kwa Hong Kong. Uingereza imesema sheria hiyo inaweza kukandamiza mamlaka ya ndani ya Hong Kong.

https://p.dw.com/p/3cutE
Hongkong Proteste Gesetz Nationalhymne Festnahme
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Cheung

Hisia mbalimbali zinazidi kutolewa kufuatia hatua ya bunge la China kuidhinisha mipango ya sheria tete ya usalama kwa Hong Kong. Waziri Mkuu wa China Li Keqiang amesema sheria hiyo mpya inalenga kuulinda mji wa Hong Kong, lakini Japan, Marekani, Canada, Australia na hata Marekani zimeikosoa hatua hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Japan imesema ina wasiwasi mwingi kuhusu hatua ya China kuidhinisha sheria hiyo ambayo wachambuzi wamehofia inaweza kuhatarisha utawala spesheli wa ndani na uhuru wa Hong Kong.

Wizara hiyo imemuita balozi wa China mjini Tokyo kumueleza mtizamo wao kuhusu sheria hiyo na kuongeza kuwa itafuatilia kwa karibu matukio yatakayofuata.

Makubaliano ya kuwepo taifa moja lakini mifumo miwili yanatishiwa?

Katika taarifa ya nadra, punde tu baada ya sheria hiyo kupitishwa, wizara ya mambo ya nje ya Japan imeutaja mji wa Hong Kong kama mshirika muhimu zaidi. Yoshihide Suga ambaye ni waziri mwenye hadhi ya juu katika baraza la serikali la Japan amesema:

"Hong Kong ni mshirika muhimu zaidi ambaye tuna mahusiano makubwa kibiashara na hata baina ya watu. Tunafikiri ipo haja ya kuwepo hatua za maendeleo kidemokrasia, chini ya utaratibu wa taifa moja mifumo miwili. Mfumo wa sasa ulio huru na wazi unapaswa kuendelea."

China imesema kuwa sheria yake ya usalama wa taifa kwa Hong Kong inanuia kuimarisha uthabiti na ustawi wa muda mrefu wa mji huo lakini pia kuwaadhibu wanaodhoofisha nguvu ya dola.
China imesema kuwa sheria yake ya usalama wa taifa kwa Hong Kong inanuia kuimarisha uthabiti na ustawi wa muda mrefu wa mji huo lakini pia kuwaadhibu wanaodhoofisha nguvu ya dola.Picha: Getty Images/A. Kwang

Serikali ya Uingereza ina wasiwasi mwingi kuhusu sheria ya China juu ya usalama wa Hong Kong, hali inayotishia kuenda kinyume na utaratibu wa taifa moja lakini mifumo miwili. Amesema waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab.

China yaitetea sheria yenye utata

Lakini waziri Mkuu wa China Li Keqiang, amesema sheria hiyo inalenga kulinda utulivu wa muda mrefu wa mji huo na maendeleo yake.

Li ameongeza kuwa sheria hiyo yenye utata inayolenga kukabili visa vya ugaidi, uvunjifu wa sheria, miingilio kutoka nje na miito ya kutaka kujitenga, imetungwa kwa njia ya kuheshimu makubaliano ya kupowe taifa moja lakini mifumo miwili.

Mkataba huo uliokubaliwa mwaka 1997 kati ya China na Uingereza, unasema Hong Kong ambayo ni koloni la zamani la Uingereza inapaswa kuwa na kiwango fulani cha mamlaka yake ya ndani nje ya China hadi mwaka 2047.

Wachambuzi wanahoji kuwa kwa China kulipita bunge la Hong Kong kwa kutumia sheria ya usalama wa taifa, ni kuayafanya makubaliano ya awali kukosa maana.

Vyanzo: RTRE, DPAE