Sheria ya kijeshi Ukraine yampa wasiwasi Putin
28 Novemba 2018Jumapili iliyopita walinzi wa mpakani wa Urusi walizifyatulia risasi meli za kivita na baadae kuziteka pamoja na mabaharia wake. Sudi Mnette anaarifu zaidi kuhusu mzozo huo wa Ukraine na Urusi.
Jana Jumatatu serikali ya Ukraine ilitangaza sheria ya kijeshi katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa kuna ongezeko la vitisho vya kushambuliwa kutoka Urusi. Rais Petro Poroshenko alisema sheria hiyo ni muhimu ili kuimarisha ulinzi wa Ukraine baada ya Urusi kukamata meli za wanamaji wa Ukraine karibu na eneo la Crimea na kuwashikilia mabaharia wake mateka.
Mazungumzo ya Putin na Merkel
Katika taarifa ya awali ya mapema leo serikali ya Kremlin imesema Rais Putin alielezea hali ya kuongezeka kwa wasiwasi wake na kitendo hicho cha kuwekwa kwa kuweka sheria ya kijeshi. Katika mazungumzo yake kiongozi huyo kwa njia ya simu na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema anayaelekeza malalamiko yote kwa Ukraine na kuongeza kuwa wanafanya vitendo hivyo kwa sababu za kisiasa.
Lakini kwa mujibu wa Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert, alisema kwenye mazungzmzo hayo Merkel alisisitiza, uhitaji wa kusitisha mvurugano na mazungumzon ya amani.
Sauti za mateka wa Ukraine
Katika hatua nyingine shirika la kijasusi nchini Urusi limesambaza video inayowaonesha wanajeshi watatu wa majini wa Urusi waliokuwemo katika miongoni mwa meli za Ukraine, zilizotekwa Jumapili. Shirika hilo ambalo kwa ufupi linafahamika kama FSB liliitoa video hiyo, likionesha mabaharia hao wakihojiwa, ambao wote kwa pamoja walithibitsha kukiuka sheria za mpakani za Urusi. Haikuweza kufahamika mara moja kama kama watu hao walikuwa wakizungumza kwa shinikozo. Mmoja miongoni mwao alionekana akisoma maneno aliyokuwa akiyasema kupitia kielezo fulani machoni mwa sura yake.
Kwa upande wake mshirika wa sasa wa Urusi, Uturuki ametoa wito wa kutaka mvutano baina ya mataifa hayo mawili kumalizwa kwa njia ya mazungumzo. Aidha wito kama huo umetolewa na Waziri wa mambo ya Nje wa Austria Karin Kneissl akisisitiza umuhimu wa mzozo huo kutatuliwa bila matumizi ya silaha.
Duru katika eneo hilo zinaeleza kuwa mapigano ya kijeshi ya Jumapili yalikuwa ya kwanza katika makabiliano kati ya Urusi na Ukraine.
Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman