Sheria ya hali ya hatari Ethiopia na Migodi Magazetini
23 Februari 2018Tunaanzia nchini Ethiopia ambako kishindo cha wananchi barabarani kimepelekea waziri mkuu wa nchi hiyo Hailemariam Desalegn kuamua kujiuzulu."Kura ya kutokua na imani na serikali" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la Frankfurter Allgemeine kuhusu zahma inayopiga katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika. Gazeti linahisi uamuzi wake wa kuwaachilia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa ndio chanzo cha kulazimika Desalegn kujizulu. Franfurter Allgemeine linajiuliza kama sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa itawazuwia wananchi kuteremka majiani kudai mageuzi ya kidemokrasia na haki.
Sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa siku moja baada ya Hailemariam Desalegn kutangaza kwamba anajiuzulu ni ya pili katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, linakumbusha Frankfurter Allgemeine na kuutaja uamuzi huo wa serikali kuwa ni ishara ya mpasuko na hali ya kutojiamini miongoni mwa viongozi wa nchi hiyo. Jamii za watu wa makabila ya Oromo na Amhara, wanaowakilisha thuluthi mbili ya wakaazi jumla wa Ethiopia, wanahisi wanadhulumiwa na watu wa kabila la Tigrinya ambao ingawa ni asili mia sita tu ya wakaazi jumla, lakini wanadhibiti nyadhifa zote za juu serikalini, jeshini na pia katika vikosi vya usalama.
Hali ya Ethiopia inafuatiliziwa pia katika nchi jirani
Frankfurter Allgemeine linamaliza kwa kukumbusha kilio cha makundi 120 ya kikabila yanayodai utawala wa ndani na wengine wanaodai uhuru pamoja na mapigano ya mara kwa mara ya kuania ardhi . Matukio nchini Ethiopia yanafuatiliziwa kwa makini katika nchi jirani za Sudan Kusini, Somalia na mpaka Kenya ikikumbukwa kwamba Ethiopia ilikuwa ikisifiwa kama mfano wa utulivu katika pembe ya Afrika.
Hali nchini Ethiopia imeripotiwa pia na mhariri wa gazeti la mjini Berlin die Tageszeitung anaemulika zaidi kinyang'anyuro cha kuania madaraka katika nchi hiyo inaotawaliwa kwa mkono wa chuma.
Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo kuwatoza malipo ziada wachimba migodi
Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo pia imegonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani wiki hii. Makampuni yanayochimba mali ghafi yanakabiliwa na mashaka katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Frankfurter Allgemeine linalozungumzia azma ya serikali kuzidisha malipo kwa makampuni hayo kuweza kupata liseni za kuendesha shughuli zao. Mapema mwaka huu bunge la mjini Kinshasa limezifanyia marekebisho sheria zinazohusiana na mali ghafi. Pindi sheria hizo zikianza kufanya kazi basi makampuni yanayochimba migodi nchini humo naiwe Glencore, Randgold Resources au Ivanhoe Mines yatalazimika kulipia zaidi liseni zao. Kwasababu malipo ya kupata liseni za kuchimba maadini mfano ya dhahabu, shaba au kobalt yanasemekana yataongezeka kupita kiasi.
Zaidi ya hayo jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo inapanga kuanzisha kodi ya "mapato ya juu" ikimaanisha bei ya maadini inapopanda katika soko la dunia na kupindukia kiwango fulani, wenye kuchimba madini hayo watalazimika kulipa kodi ziada. Frankfurter Allgemeine linakumbusha asili mia 60 ya madini ya Kobalt duniani inapatikana katika ardhi ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na bei ya madini hayo katika soko la dunia imeongezeka mara tatu tangu msimu wa kiangazi mwaka 2016. Viongozi wa makampuni yanayochimba migodi, wanazingatia kwa makini hatua zinazotaka kuchukuliwa na serikali.
Glencore latishia kushitaki dhidi ya sheria mpya
Mwenyekiti wa Glencore, kampuni lililotajwa katika ripoti iliyofichua majina ya wanaohusika na visa vya rushwa inayojulikana kama "Paradise Papers" ameshaonana na rais Joseph Kabila ambae ndie atakaeidhinisha sheria hizo mpya. Hata hivyo juhudi zake sawa na za wenzake hazikuleta tija mpaya sasa. Mwenyekiti wa Glenore, Ivan Glasenberg anasema hajakata tamaa, mazungumzo yanaendelea, lakini pindi wakishindwa moja kwa moja, Frankfurter Allgemeine linasema hawatakuwa na njia nyengine isipokuwa kutumia njia za kisheria dhidi ya sheria hizo mpya. Frankfurter Allgemeine linakumbusha jinsi bei ya maadini ya thamani ilivyoongezeka: Faida taaslim imeongezeka mara nne na kufikia dala bilioni 5.8
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL
Mhariri:Yusuf Saumu